• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
ODM yaomba mbunge wa Maragua msamaha

ODM yaomba mbunge wa Maragua msamaha

CHARLES WASONGA na MWANGI MUIRURI

CHAMA cha ODM kimemuomba msamaha Mbunge wa Maragua Mary Wamaua kufuatia kisa ambapo alidhulumiwa na walinda usalama katika mkutano wa Azimio la Umoja Ijumaa.

Kwenye video iliyosambaa mitandaoni siku hiyo Bi Wamaua alionekana akibishana na walinda usalama katika lango la kuingia watu mashuhuri katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi ambako mkutano huo ulifanyika. Hii ni baada ya mmoja wao kuonekana akijaribu kumsukuma asitumie lango hilo.

Huku akionekana mwenye hasira Bi Wamaua alisisika akisema: ‘Mkifika State House itakuwa namna gani?…Mimi ni mbunge aliyechaguliwa na watu wa Maragua na mnanisukuma kama gunia la viazi…mtatupata Murang’a’.Lakini kupitia taarifa kwa vyombo vya habari jana, mwenyekiti wa ODM John Mbadi alimuomba msahama Bi Wamaua akisema chama hicho kinasikitikia kitendo hicho.

Bw Mbadi ambaye ni mbunge wa Suna Kusini alitoa hakikisho kwamba kitendo kama hicho hakitatokea tena.’Kwa niaba ya chama cha ODM, ningependa kumwomba msamaha hadharani kwa Mheshimiwa Wamaua kufuatia kisa ambapo alidhulumiwa na maafisa wa usalama alipotaka kuingia katika uwanja wa Kasarani kuhudhuria Mkutano wa Azimio la Umoja,”Kwa sababu ulikuwa mkutano ambapo kiongozi wa chama chama chetu alitoa tangazo muhimu kuhusu mipango yake ya kisiasa, tunasema pole sana,’ akasema Bw Mbadi.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ndiye kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa alisema Bw Odinga ni mtetezi wa haki za wanawake na hawezi kuvumilia vitendo vya dhuluma dhidi yao.’Kama chama tutafanya kila tuwezalo kutetea haki za wanawake nyakati zote na bila kuzingatia hadhi yao katika jamii,’ Bw Mbadi akasisitiza huku akiwarai wakazi wa Maragua kukubali ombi lao.

Baada ya tukio hilo, viongozi kutoka kaunti ya Murang’a walilaani kitendo hicho wakisema walinda usalama hawakufaa kumkosea heshima mbunge huyo.Mbunge wa Kandara Alice Wahome na mbunge wa zamani wa Maragua Elius Mbau walisema kitendo hicho ‘cha kinyama’ ni ishara ya dharau kwa watu wa Maragua na eneo la Mlima Kenya kwa ujumla.

‘Hii ni mojawapo ya sababu tunawahimiza watu wa Mlima Kenya kutohadaiwa kuunga mkono mrengo huo wa kisiasa. Nembo kuu ya ODM ni fujo,’ akasema Bi Wahome ambaye ni mfuasi sugu wa Naibu Rais William Ruto.Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanawake tawi la Mlima Kenya Bi Lucy Nyambura alisema:

‘Ni kinaya kwamba wanaojifanya kuendeleza ajenda ya kuunganisha taifa hili wanawabagua watu kutoka maeneo mengine ya nchi.’Bi Wamaua ni miongoni mwa wabunge wachache kutoka Mlima Kenya ambao wamekataa kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto.Ameamua kusalia ndani ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Wandani wa Ruto: Raila atasalitiwa

Uhuru aapa kuwa BBI itatimia

T L