• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Rais Ruto afanya mabadiliko yaliyowaathiri Makatibu saba wa Wizara

Rais Ruto afanya mabadiliko yaliyowaathiri Makatibu saba wa Wizara

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amefanya mabadiliko yanayowaathiri makatibu saba wa wizara baada ya kumfuta kazi Katibu katika Wizara ya Afya aliyesimamia Idara ya Afya ya Umma Josephine Mburu.

Bi Mburu alipigwa kalamu Jumatatu kuhusiana na sakata ya ununuzi wa neti za kuzuia mbu za thamani ya Sh4 bilioni katika Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA).

Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Magereza Mary Muthoni amehamishwa kuchukua nafasi ya Bi Mburu huku nafasi yake (Muthoni) ikipewa Esther Ngeno ambaye alikuwa Katibu katika Afisi ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Katibu wa Afya anayesimamia Idara ya Afya ya Matibabu Mhandisi Peter Tum, aliyesimamia mamlaka ya Kemsa, amesazwa kufutwa kazi na badala yake amehamishwa hadi Wizara ya Michezo, Masuala ya Vijana na Sanaa.

Katibu wa Idara ya Mifugo Harry Kimtai amehamishwa kuchukua nafasi ya Mhandisi Tum huku aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Michezo Jonathan Mueke akichukua nafasi ya Bw Kimtai.

Katibu wa Idara ya Misitu Ephantus Kimani amebadilishana nafasi na mwenzake wa Unyunyiziaji Gitonga Mugambi.

Rais Ruto amempendekeza Faith Njeri Harrison kuwa Katibu katika Afisi ya Mkuu wa Mawaziri kuchukua nafasi ya Bi Ngeno.

Bi Harrison ambaye zamani alihudumu kama Afisa Mkuu katika Idara ya Fedha, Kaunti ya Kiambu sasa atapigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Usalama na Utawala ili kubaini ufaafu wake wa cheo hicho.

Mabadiliko hayo yanajiri baada ya mkutano wa baraza la Mawaziri uliofanyika Jumanne, Mei 16, 2023 ambapo Rais Ruto alihimiza uzingativu wa maadili miongoni mwa maafisa wanaohudumu katika Wizara na Idara za Serikali.

“Alitoa onyo kali dhidi ya maafisa wa serikali kujiingiza katika ufisadi na ubadhirifu wanapotoa hudumu kwa wananchi. Rais aliwataka mawaziri kuheshimu wajibu wao wa Kikatiba kwa wananchi. Alikariri kuwa ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za umma hautavumiliwa,” ikasema taarifa kutoka Afisa ya Masuala ya Mawaziri baada ya mkutano huo.

Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa mkutano huo ulikubaliana kuhusu haja ya matumizi mazuri ya rasilimali za umma.

Mabadiliko ambayo Rais Ruto alifanya Jumanne, Mei 16, 2023 ndio ya kwanza kwake kufanya katika serikali yake tangu alipoingia afisini Septemba 13, 2022.

  • Tags

You can share this post!

SIHA NA LISHE: Fahamu mlo sahihi ikiwa wewe ni...

UEFA: Manchester City na Real Madrid kumaliza udhia leo...

T L