• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Simba jike atishia kuangusha Ripoti ya Kamati ya Maridhiano endapo haitaangazia matakwa ya Mlima Kenya

Simba jike atishia kuangusha Ripoti ya Kamati ya Maridhiano endapo haitaangazia matakwa ya Mlima Kenya

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ametishia kuangusha Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Maridhiano (NADCO) itakapowasilishwa bungeni, endapo haitaangazia matakwa ya jamii ya Mlima Kenya.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tikiti ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) japo anatofautiana na serikali ya Rais William Ruto, amesisitiza kwamba ripoti hiyo sharti iangazie masuala yanayohusu jamii anayotoka.

Akizungumza kwenye hafla ya mazishi, mwanasiasa huyo jasiri alisisitiza kwamba ugavi wa raslimali za umma unapaswa kusambazwa kwa mujibu wa idadi ya watu.

Alikuwa akirejelea kigezo cha ‘mtu mmoja-kura moja-shilingi moja’.

Bi Wamuchomba alisema mkondo huo katika ugavi wa raslimali za umma, ndio utasaidia kuangazia changamoto zinazokumba maeneo.

“Mazungumzo au majadiliano yoyote mezani, hoja yetu ni mtu mmoja, kura moja, shilingi moja. Nilizungumzia hilo, nikaambiwa ninyamaze. Mwaka mmoja sasa umepita. Tumegawa basari (ufadhili wa masomo unaotolewa kupitia Fedha za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge – NG-CDF) kwa mara ya kwanza, tunangojea raundi ya pili. Ni haki ninyamaze mkiteseka?” Wamuchomba akataka kujua.

Mbunge huyo ambaye kati ya 2017 hadi 2022 alihudumu kama Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Kiambu, alitahadharisha kwamba endapo NADCO haitaainisha hoja za Mlima Kenya, basi hatakuwa na budi ila kushawishi wabunge wenzake kuangusha ripoti hiyo itakapowalishwa bungeni kujadiliwa ili kupitishwa kuwa sheria au kuangushwa.

Ripoti hiyo ya Mazungumzo ya Maridhaino kati ya Serikali ya Kenya Kwanza na muungano wa upinzani – Azimio la Umoja, iliandaliwa na mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wah (akiwakilisha Kenya Kwanza) na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka (Azimio).

NADCO, hata hivyo, haikuangazia jinsi ya kushusha gharama ya juu ya maisha inayozidi kulemea Wakenya.

Suala la kupunguza ushuru (VAT) unaotozwa mafuta ya petroli kutoka asilimia 16 hadi 8, na kuondoa ada ya asilimia 3 inayotozwa mfanyakazi na mwajiri, liliachiwa Rais William Ruto na kinara wa Azimio, Raila Odinga.

Wanachama wa kamati ya NADCO hawakukubaliana kuhusu hoja hizo.

Dkt Ruto na Bw Raila walikabidhiwa ripoti hiyo kwa njia ya kielektroniki.

“Hiyo ripoti ambayo Ichung’wah anataka kuleta kule bungeni…Hiyo ripoti ambayo ametengeneza akiwa na kina Kalonzo Musyoka, kama haitakuwa na maneno ya mtu mmoja, kura moja, shilingi moja, Wamuchomba anaomba ruhusa kutoka kwenu niiangushe asubuhi na mapema kama haina matakwa yetu,” Wamuchomba akasema.

Mbunge huyo wa Githunguri, Kiambu anasema ugavi wa raslimali za umma lazima utolewe kwa mujibu wa idadi ya watu kwenye maeneobunge.

 

  • Tags

You can share this post!

El Nino: Hofu nyanda za juu Pokot Magharibi mmomonyoko wa...

Naibu Gavana Kisii akabwa koo na ukoo wa Nyaribari...

T L