• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
Wakazi wa vijiji vilivyoshambuliwa Lamu watafuta maeneo salama

Wakazi wa vijiji vilivyoshambuliwa Lamu watafuta maeneo salama

NA KALUME KAZUNGU

MAUAJI ya watu wawili na magaidi wa Al-Shabaab Jumanne yanazidi kuvipaka tope vitengo vya usalama Kaunti ya Lamu kwa kuonekana kuzembea katika jukumu la kulinda maisha ya wananchi na mali.

Jumanne, dereva wa lori na msaidizi wake waliuawa kwa kuchinjwa gari lao liliposimamishwa na kundi la magaidi wa Al-Shabaab waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki eneo la Lango la Simba kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Shambulio hilo lilitekelezwa majira ya saa moja asubuhi.

Kabla ya kutekeleza mauaji hayo, magaidi wa Al-Shabaab pia walikuwa wamevamia kijiji cha Salama kati ya saa mbili unusu na saa tano usiku wa Jumatatu, ambapo waliteketeza nyumba nane na kanisa moja.

Magaidi pia waliiba mbuzi, televisheni, unga na taa za kutegemea mianzi ya jua ndani ya nyumba hizo kabla ya kuziteketeza moto.

Magaidi pia walichinja wana wa mbuzi saba na kuwaacha vijijini.

Pia walivuna mahindi changa mashambani kabla ya kutokomea msitu wa karibu.

Magaidi pia walivamia kambi ya polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) kijijini Pandanguo kilichoko umbali wa kilomita 50 kutoka kijiji cha Salama majira ya saa nane unusu alfajiri ya Jumanne lakini wakakabiliwa vilivyo na kushindwa nguvu kabla ya kutokomea msitu wa Boni.

Naibu Kamishna wa Lamu Magharibi, Gabriel Kioni alisema inaaminika magaidi walioua dereva na msaidizi wake eneo la Lango La Simba ni wale wale waliojaribu kuvamia kambi ya GSU Pandanguo.

Bw Kioni hata hivyo alisema walinda usalama wa kutosha tayari wamesambazwa kwenye maeneo husika kuwasaka na kuwamaliza waliotekeleza mavamizi hayo.

“Magaidi waliua watu wawili ambao ni dereva wa lori na msaidizi wake eneo la Lango La Simba leo Jumanne majira ya saa moja asubuhi. Kabla ya shambulio la Lango La Simba, magaidi walikuwa wamevamia kijiji cha Salama usiku na kuchoma nyumba nane na kanisa la Redeemed Gospel Church kabla ya kutorokea msituni. Pia walijaribu kuvamia kambi ya GSU Pandanguo lakini maafisa wetu wakawakabili na kuwashinda. Kwa sasa utulivu umerejea ilhali maafisa wetu wakiendeleza uchunguzi. Wananchi waondoe hofu,” akasema Bw Kioni.

Kufuatia mashambulio hayo ya Jumatatu na Jumanne, taharuki imetanda kwenye vijiji vya Salama, Pandanguo, Jima na viungani mwake baadhi ya wakazi wakishuhudiwa kuhama vijiji hivyo kwa kuhofia usalama wao.

Kuna wale waliotorokea kwenye kambi ya wakimbizi ya Shule ya Msingi ya Juhudi, Lamu Magharibi ilhali wengine wakitorokea mijini, ikiwemo Mpeketoni, Kibaoni na Witu.

Wakazi walisema katu hawana imani na idara ya usalama kwani ni dhahiri kwamba imezembea katika kukabiliana na magaidi vijijini mwao.

Peter Muthengi ambaye ni askofu wa kanisa lililochomwa la Redeemed Gospel Church kijijini Salama alisema amepoteza mali ya thamani ya zaidi ya Sh300,000 kwenye shambulio la Jumatatu usiku.

“Nilikuwa na vipaza sauti, viti na mali nyingine ipatayo karibu laki tatu. Vyote vimegeuzwa jivu na magaidi. Serikali izingatie kilio chetu cha kambi ya walinda usalama iwekwe eneo hili. Tumechoka kupoteza maisha ya watu na mali,” akasema Bw Muthengi.

Mary Wanjiku alihoji kwa nini magaidi wa Al-Shabaab wanaendelea kutawala kwenye vijiji vya Lamu wakati ambapo kila mara kumeshuhudiwa opereshyeni na doria za walinda usalama eneo hilo.

“Ipo haja ya serikali ijitokeze kinagaubaga kutueleza ni vipi hili suala la usalama litakabiliwa na kumalizwa. Ni dhahiri hawa Al-Shabaab wamewashinda akili ilhali sisi tukiendelea kuumia vijijini mwetu,” akasema Bi Wanjiku.

Kati ya Juni na Agosti mwaka huu, kaunti ya Lamu imepoteza jumla ya watu kumi ilhali mali ya mamilioni ya fedha ikiangamia mikonono mwa magaidi wa Al-Shabaab.

Jumanne wiki iliyopita, watu wanane walinusurika kifo pale magaidi wa Al-Shabaab walipotekeleza uvamizi mara mbili eneo la Koreni na kwenye barabara ya Hindi kuelekea Bar’goni majira ya asubuhi.

Agosti 1, 2023, magaidi zaidi ya 60 wa Al-Shabaab walivamia magari ya wapita njia eneo la Mwembeni, karibu na Lango La Simba kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. Mke wa Diwani wa Hindi James Njaaga na mhudumu wa bodaboda waliuawa kwenye shambulio hilo la majira ya saa mbili kasoro dakika 20 asubuhi lililoacha wengine 10, akiwemo Bw Njaaga wakiuguza majeraha.

Gari moja na pikipiki mbili ziliteketezwa na magaidi hao wa Al-Shabaab.

Julai 12, 2023, mtu mmoja aliuawa na nyumba sita zikachomwa kwenye vijiji vya Salama Block 17 na Widho vilivyoko Lamu Magharibi.

Juni 24, 2023, magaidi wa Al-Shabaab walivamia vijiji nvya Salama na Juhudi ambapo waliwachinja na kuwaua wanaume 5 na kuteketeza nyumba sita.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yarudishia Pasta Ezekiel nyota yake

Nyota 5 kuwakilisha Kenya kwenye Mashindano ya Dunia ya...

T L