• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Ebola: ‘Lockdown’ yanukia Kampala

Ebola: ‘Lockdown’ yanukia Kampala

KAMPALA, UGANDA

NA JONATHAN KAMOGA

HOFU imetanda kuhusu uwezekano wa kutangazwa kwa “lockdown” jijini Kampala, Uganda kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Waziri wa Afya Dkt Jane Ruth Aceng jana Jumamosi alisema wahudumu wa afya wanaendesha operesheni ya kusaka zaidi ya watu 300 waliotangamana na wagonjwa wa Ebola, wengi wao wakiwa jijini Kampala na wilaya jirani ya Wakiso.

Polisi na wanajeshi wamefunga maeneo mbalimbali ya umma kama vile maegesho ya teksi, masoko ya wazi, vituo vya mabasi ya uchukuzi wa abiria.

Baadhi ya maduka, mikahawa na maeneo mengine ya umma yamerejesha sharti la watu kuvalia barakoa na kunawa mikono kabla ya kuingia humo.

Baadhi ya mashirika ya kibinafsi nayo yamewaamuru wafanyakazi wao kurejelea mtindo wa kufanya kazi kutoka nyumbani.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema msambao wa Ebola kutoka eneo la Kati mwa Uganda, ambako iligunduliwa kwanza, hadi maeneo mengine, umeibua hofu.

Alisema juhudi zinapasa kuendeshwa za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya watu 30 tangu mwezi Septemba.

Wiki hii, Bunge la Uganda liliamua kwamba ni wabunge 200 pekee, kati ya 500, wataruhusiwa kuketi ukumbini, ili kupunguza kuenea kwa Ebola.

Wizara ya Afya pia ilithibitisha visa sita vya maambukizi katika shule tatu jijini Kampala huku ikisaka zaidi ya watu 170 wanaoaminika kutangamana na wagonjwa hao.

Hata hivyo, shule hizo ambazo hazikutajwa, hazikufungwa.

Dkt Aceng alisema watu wote waliotangamana na wagonjwa wa Ebola jijini Kampala watazuiliwa katika karantini kwa siku 21.

  • Tags

You can share this post!

WALIOBOBEA: ‘Sirkal’ alipokataa wadhifa serikalini

Brighton wapepeta Chelsea katika kipute cha EPL ugani Amex

T L