• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Brighton wapepeta Chelsea katika kipute cha EPL ugani Amex

Brighton wapepeta Chelsea katika kipute cha EPL ugani Amex

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Chelsea, Graham Potter, amesema “hana chochote cha kusikitikia” baada ya mashabiki wa Brighton kumpokea kwa cheche za matusi na maneno ya chuki wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia waajiri wake Chelsea wakipepetwa 4-1 ugani Amex mnamo Jumamosi.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Potter kurejea ugani Amex kukabiliana na waajiri wake wa zamani waliomwachilia ajiunge na Chelsea kujaza nafasi ya kocha Thomas Tuchel mnamo Septemba 2022.

Chini ya Potter, Brighton walikamilisha kampeni ya EPL katika nafasi ya tisa mnamo 2021-22, hiyo ikiwa nambari nzuri zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kushikilia katika historia yao ligini. Hata hivyo, aliagana nao baada ya kusimamia mechi sita pekee za EPL muhula huu.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 52 alizomwa na mashabiki wa Brighton hata kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mchezo kupulizwa.

Leandro Trossard aliwaweka Brighton kifua mbele kunako dakika ya tano kabla ya Ruben Loftus-Cheek na Trevoh Chalobah kujifunga na hivyo kufanya mambo kuwa 3-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Ingawa Kai Havertz alirejesha Chelsea mchezoni kwa kufunga bao baada ya kushirikiana na Conor Gallagher mwanzoni mwa kipindi cha pili, Pascal Gross alizamisha kabisa chombo cha wageni wao katika dakika ya 90. Bao hilo lilikuwa zao la kipa Edouard Mendy wa Chelsea kubabatizwa na kombora la Julio Enciso.

Brighton walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kutoshinda mechi yoyote kati ya tano walizozipiga baada ya Potter kuondoka ugani Amex mnamo Septemba 2022.

Ni Glenn Murray na Neal Maupay ambao wamefungia Brighton idadi kubwa zaidi ya mabao ya EPL kuliko Trossard ambaye sasa amepachikia waajiri wake magoli 25 ligini. Bao dhidi ya Chelsea lilimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufungia Brighton mabao matano ligini chini ya mkufunzi mpya.

Ushindi wa Brighton ulikuwa wao wa kwanza dhidi ya Chelsea katika EPL. Hadi walipokutana, Chelsea walikuwa wameshinda mechi 10 na kuambulia sare mara nne kutokana na mechi 14 za awali dhidi ya Brighton katika EPL.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Leicester 0-1 Man-City

Bournemouth 2-3 Tottenham

Brentford 1-1 Wolves

Brighton 4-1 Chelsea

Crystal Palace 1-0 Southampton

Newcastle 4-0 Aston Villa

Fulham 0-0 Everton

Liverpool 1-2 Leeds

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ebola: ‘Lockdown’ yanukia Kampala

Leeds United wacharaza Liverpool uwanjani Anfield na...

T L