• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
Ebola: Uganda sasa yaweka ‘lockdown’

Ebola: Uganda sasa yaweka ‘lockdown’

NA DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

UGANDA imefunga na kusimamisha shughuli zote zinazohusu mwingiliano wa watu (lockdown) katika wilaya mbili kwa wiki tatu zijazo, huku maambukizi ya maradhi ya Ebola yakiendelea kuongezeka.

Hapo jana Jumapili, serikali ilisema kuwa maeneo yote ya burudani na kuabudia yatafungwa katika wilaya za Mubende na Kassanda, huku pia ikiweka kafyu.

Hatua hiyo inaonekana kuwa kinyume na msimamo wa awali wa Rais Yoweri Museveni, aliyesema kuwa hakukuwa na hitaji la utekelezaji wa hatua kama hizo.

Kufikia sasa, watu 19 wamethibitishwa kufariki nchini humo kutokana na ugonjwa huo, huku hali ya watu 58 ikifuatiliwa na taasisi mbalimbali za afya, kubaini ikiwa wameambukizwa maradhi hayo au la.

Maradhi hayo yalianzia katika wilaya ya Mubende mapema mwezi Septemba.

Wilaya hiyo iko umbali wa kilomita 80 kutoka jiji kuu, Kampala.

Mwanzoni, Rais Museveni aliondoa uwezekano wowote wa kufunga maeneo hayo, akisema maradhi hayasambazwi kwa njia ya kupumua kama ilivyo kwa Covid-19.

Alisema hakukuhitajika masharti kama yale yaliyowekwa wakati wa janga la Covid-19.

Lakini mnamo Jumamosi, kiongozi huyo alisimamisha shughuli na safari zozote katika wilaya hizo kwa muda wa siku 21 zijazo.

Licha ya masharti hayo, matrela ya kusafirisha mizigo bado yataruhusiwa kuingia ama kutoka katika maeneo hayo. Hata hivyo, mifumo mingine yote ya usafiri imesimamishwa.

“Hizi ni juhudi za muda zinazokusudiwa kudhibiti maambukizi ya Ebola,” akasema, kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.

“Sote tunafaa kushirikiana na idara zote husika ili kumaliza janga hili haraka iwezekanavyo.”

Tayari, Rais Museveni amewaagiza polisi kumkamata mtu yeyote anayedaiwa kuwa na maradhi hayo na anakataa kujitenga.

Pia, amewazuia madaktari wa matibabu ya kiasili dhidi ya kuwahudumia watu wanaodaiwa kuwa na virusi hivyo.

Katika mikurupuko ya hapo awali ya maradhi hayo, madaktari hao wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwa chanzo cha kusambaa kwake.

Kifo cha kwanza kilichotokana na maradhi kilimhusisha mwanamume aliyekuwa na umri wa miaka 24 katika wilaya ya Mubende. Jamaa wake sita pia walifariki.

Baadaye, maradhi hayo yalifika jijini Kampala, ambapo mtu mmoja aliripotiwa kufariki mnamo Oktoba.

Hata hivyo, maafisa wa afya wamekuwa wakisisitiza kuwa maradhi hayo bado hayajafika jijini humo, kwani mwathiriwa alikuwa amesafiri kutoka wilaya ya Mubende.

Mkurupuko wa sasa unahusishwa na virusi aina ya Sudan, ambavyo ni sugu kwa chanjo yoyote dhidi yake iliyopatikana.

Ni virusi vya Ebola aina ya Zaire pekee ambavyo vina chanjo maalum.

Aina hiyo ya Ebola ndiyo iliyosababisha maafa ya zaidi ya watu 11,000 katika eneo la Afrika Magharibi kati ya 2013 na 2016.

Maradhi hayo husambazwa kupitia mwingiliano wa majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa.

Baadhi ya dalili zake ni kutapika, kuendesha na kuvuja damu miongoni mwa baadhi ya sehemu za ndani ya mwili.

Mwathiriwa anaweza kukaa kati ya siku mbili na wiki tatu kabla ya makali yake kuanza kujitokeza.

Maradhi hayo pia yanahusishwa na magonjwa kama malaria na homa ya matumbo.

  • Tags

You can share this post!

9 kutoa ushahidi wa madai ya wizi wa kura Kwale

MWALIMU WA WIKI: Nyimbo na maigizo ni siri yake darasani

T L