• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Hisia mseto Sri Lanka ikipata rais mpya

Hisia mseto Sri Lanka ikipata rais mpya

NA MASHIRIKA

COLOMBO, SRI LANKA

WABUNGE nchini Sri Lanka wamemchagua Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe kuwa rais mpya wa taifa hilo.

Hii ni licha ya kiongozi huyo kutokuwa maarufu miongoni mwa raia.

Wickremesinghe anakabiliwa na kibarua kigumu cha kurejesha hali ya kawaida nchini humo, baada yake kukumbwa na maandamano ya miezi kadhaa.

Wickremesinghe alimshinda mpinzani wake mkuu, Dullus Alahapperuma, kwa kuzoa kura 134 dhidi ya kura 82 kwenye Bunge la Kitaifa.

Aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Gotabaya Rajapaska, alitoroka taifa hilo wiki iliyopita.

Kwanza, alitorokea katika kisiwa cha Maldives na baadaye nchini Singapore, baada ya maelfu ya waandamanaji kuvamia makazi yake rasmi kati ya majengo mengine ya serikali.

Waandamanaji hao pia walikuwa wakimshinikiza Wickremesinghe kujiuzulu, ikizingatiwa yeye ni mshirika wa karibu wa familia ya Rais Rajapaska.

Aliteuliwa kuhudumu kama waziri mkuu mnamo Mei.

Waandamanaji walichoma makazi yake wiki iliyopita huku pia wakivamia afisi yake kama waziri mkuu, jijini Colombo.

Maelfu ya raia wamekuwa wakiandamana nchini humo kwa miezi kadhaa kutokana na hali mbaya na uchumi.

Taifa hilo limekuwa likikumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, mafuta na bidhaa nyingine za msingi.

Baada ya kuchaguliwa kwake, Wickremesinghe, aliwaambia wabunge kwamba nchi hiyo iko “katika hali mbaya sana.”

Alikubali kuwa “anakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kiuchumi.”

Wickremesinghe, 73, vile vile aliwarai washindani wake wa kisiasa kushirikiana na serikali yake kwa manufaa ya taifa hilo.

Wengi walisema wanatarajia kuchaguliwa kwake kutarejesha uthabiti wa kisiasa nchini humo.

Hilo linatarajiwa kuisaidia nchi hiyo kufanya mazungumzo na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kulipa msaada wa kifedha ili kufufua uchumi wake.

Tayari, kiongozi huyo alikuwa ashaanza mazungumzo hayo mwezi uliopita, alipokuwa akihudumu kama Waziri Mkuu.

Chama tawala nchini humo, Sri Lanka Podujana Peramnua Party, kilisema kuwa wabunge wake wengi walimuunga mkono Wickremesinghe kutokana na rekodi yake katika kuboresha uchumi.

“Tunahisi kuwa Ranil Wickremesinghe ndiye kiongozi wa kipekee mwenye tajiriba na uwezo wa kutoa suluhisho kwa changamoto za kiuchumi zinazotukumba,” akasema Katibu Mkuu wa chama hicho, Sagara Kariyawasam.

Wickremesinghe amehudumu kama waziri mkuu kwa vipindi sita.

Kijumla, amekuwa kwenye ulingo wa siasa nchini humo kwa jumla ya miaka 45.

Hata hivyo, hapendwi na wananchi wengi, kwani wanamwona kama sehemu ya uongozi uliokuwepo.

Baadhi ya wadadisi wanasema huenda kuchaguliwa kwake kukazua maandamano zaidi.

Kabla ya kuchaguliwa kwake, baadhi ya waandamanaji walichoma magurudumu ya magari na kuyaweka kwenye barabara zinazoelekea bungeni.

Hata hivyo, maandamano hayo hayakuwa makubwa kama siku za hapo awali.

Baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa, baadhi yao waliandamana kwenye barabara kuu jijini Colombo wakipinga kuchaguliwa kwake.

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wa Man Utd wafokea nahodha Maguire licha ya klabu...

Matiang’i aonya viongozi dhidi ya kufadhili magenge...

T L