• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Wasiwasi Urusi ikifanya ushauri na Afrika Kusini

Wasiwasi Urusi ikifanya ushauri na Afrika Kusini

NA MASHIRIKA

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

HOFU imeibuka baada ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, kuzuru nchini Afrika Kusini jana Jumatatu, kwa mazungumzo na mojawapo ya washirika wake wa karibu zaidi barani Afrika.

Tangu Urusi kuivamia Ukraine mwezi Februari 2022, Afrika imegawanyika kuhusu uvamizi huo na juhudi za baadhi ya mataifa ya Magharibi kuitenga Urusi.

Lavrov alikutana na mwenzake wa Afrika Kusini, Nalendi Pandor, baada ya kukutana na viongozi wa vyama kadhaa vya upinzani.

Hata hivyo, raia wa Ukraine wanaoishi Afrika Kusini wamekashifu vikali ziara hiyo kama “isiyofaa”.Mawaziri hao wawili waliwahutubia wanahabari ijapokuwa baadaye walifanya mazungumzo ya faraghani.

Serikali ya Rais Cyril Ramaphosa imekuwa ikisisitiza kuwa Afrika Kusini haiungi mkono nchi yoyote kwenye mzozo unaoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

“Kama Afrika Kusini, msimamo wetu ni kuunga mkono michakato yote ya kutafuta amani katika mapigano yanayoendelea barani Afrika na duniani kote kwa jumla,” akasema Pandor.

Afrika kusini haina ushirikiano mkubwa wa kibiashara na Urusi, ijapokuwa mwegemeo wake wa kisiasa na masuala tofauti duniani umekuwa ukiunga mkono pakubwa na Urusi na China.

Mataifa hayo mawili yamekuwa yakiendesha juhudi za kupunguza ushawishi wa kisiasa na kiuchumi wa Amerika duniani.

Pandor amekuwa akisisitiza kuwa Afrika Kusini haitaingilia kati mzozo huo, ijapokuwa imeyalaumu vikali mataifa ya Magharibi kwa kuitenga na kuiwekea vikwazo Urusi, huku yakipuuza mzozo unaoendelea baina ya Israeli na Palestina.

Afrika Kusini imekuwa ikidinda kushiriki kwenye shughuli za upigaji kura kuhusu mzozo huo katika vikao vya Umoja wa Mataifa (UN).

Hata hivyo, imekuwa ikidumisha urafiki wa karibu na Urusi, ambayo ni rafiki wa karibu wa chama tawala cha African National Congress (ANC). Urusi ni miongoni mwa mataifa machache yaliyokuwa yakipinga utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiendelea nchini humo.

Jeshi la Afrika Kusini linatarajiwa kufanya mazoezi ya pamoja na majeshi ya Urusi na China katika eneo la pwani mwa taifa hilo kati ya Februari 17 na 27.

Ni hatua ambayo imetajwa kwamba itaathiri pakubwa urafiki baina ya Afrika Kusini na Amerika na mataifa ya Ulaya.Mazoezi hayo yatalingana na siku ambayo Urusi ilianza uvamizi wake dhidi ya Ukraine.

Urusi imekuwa ikisisitiza kuwa vita vinavyoendelea Ukraine ni “operesheni maalum ya kijeshi.”

Wiki iliyopita, jeshi la Afrika Kusini lilitaja mazoezi hayo ya pamoja kama “juhudi za kurejesha urafiki wake unaodorora baina yake na Urusi na China”.

Hapo jana Jumatatu, shirika la habari la TASS kutoka Urusi liliripoti kuwa meli ya kivita ya Urusi itakayokuwa na silaha za kisasa za kivita itashiriki kwenye mazoezi hayo.

  • Tags

You can share this post!

Chipukizi Jude Bellingham na Jamie Bynoe-Gittens wabeba...

Sambakhalu FC watwaa Lwanga Cup

T L