• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
DOUGLAS MUTUA: Waombeeni wasanii wa injili waziepuke kashfa na sakata

DOUGLAS MUTUA: Waombeeni wasanii wa injili waziepuke kashfa na sakata

NA DOUGLAS MUTUA

MARA nyingi Mtanzania mlokole anapofunga safari kuzuru Kenya hutahadharishwa kuwa kwa vyovyote vile aitunze imani yake eti kwa kuwa Kenya hakuna imani ya kweli.

Kuna mtazamo wa jumla, hasa miongoni mwa mataifa jirani, kwamba Wakenya tuna mzaha sana, hatuipi imani umuhimu na thamani inayostahili. Labda ni kweli.

Kenya ni taifa la wajanja, watu wasiojali kitu kuhusu matokeo ya baadhi ya mambo wanayofanya, mradi wananufaika kwa njia moja au nyingine.

Katika dunia hii ya wajanja kuonekana werevu, watu wanaotaka kwenda na wakati wanachukulia imani, au dini, kama kitu cha kishamba kinachowakwaza.

Mchekeshaji Eric Omondi amezuka na video tatanishi hivi majuzi akiwasuta wasanii wa injili nchini Kenya akidai wameitelekeza injili na kuingilia anasa za dunia.

Nimesalitika kuandika makala hii kwa sababu mbili: mimi ni ashiki mkubwa wa muziki, tena takriban miaka 20 iliyopita niliandikia magazeti habari za wasanii, hasa wanamuziki. Hii ina maana kwamba mada hii nina satua nayo kwa kiasi fulani, lakini usiniamini sana kwa kuwa inabadilika kila kukicha.

Ilivyo ni kwamba kawaida Wakenya hawaoni ajabu yoyote kuhusu sakata ya aina yoyote ile inapomhusisha msanii wa nyimbo za burudani. Huyo akiingia hali taabani, yake ya ndani yasimuliwe nje, kila mtu anaichukulia hiyo kuwa sehemu ya burudani, yaani kuyatumbuiza macho na masikio.

Hali hubadilika pale msanii wa nyimbo za injili anapopatikana na kashfa! Hata wasiojua uliko mlango wa kanisa au msikiti huja juu na kumkemea kwa kuiaibisha imani yake. Inaeleweka.

Ukiwa msanii wa injili, inachukuliwa kuwa mada unazoshughulikia ni za kuimarisha jamii na kuwaelekeza watu kuwa katika hali wianifu na Mungu.

Lakini naambiwa siku hizi mambo yamebadilika, sakata za kila aina – kuanzia pesa hadi ngono – zimelemea wasanii wa injili hivi kwamba wale wa burudani wamekuwa afadhali.

Tatizo kuu ni unafiki katika kila tunalofanya; msanii wa injili anapopatwa na kashfa ya unyang’anyi na kufungwa jela, tunamtetea na kudai amesingiziwa.

Mwingine anapopatikana na mke wa mtu, au katapeli watu mafedha yao, tunawasuta wanaomkashifu huku tukidai kwamba kazi ya kuhukumu ni ya Mungu.

Mungu mwenyewe alikupa akili razini za kutofautisha mazuri na mabaya, hivyo unapoliona baya ukajitia upofu kwa kuhofia kuhukumu, hilo ni kosa.

Jamii haiwezi kuendelezwa kwa unafiki wa kupuuza makosa kwa kuwa yamefanywa na watu wanaochukuliwa kuwa maarufu; uozo unaoshuhudia sasa hivi ni zao la unafiki.

Binafsi nilijua mambo yameanza kubadilika mwaka 2000 nilipowaona wasanii wa injili waliokuwa wa kizazi kipya wakati huo wakitoza watu ada za kiingilio cha shoo zao!

Hilo lilinishtua kweli kwa kuwa nilikulia katika mazingira ambapo neno la Mungu, hasa mahubiri na nyimbo zikiwa mubashara, basi hutolewa bila malipo.

Kilichofanyika kwenye shoo au mahubiri ni uuzaji wa kanda za santuri za CD au kaseti, lakini kutoza ada za kiingilio kuliachiwa watu wa disko na bendi – burudani hasa.

Kila ulipojasiria kuuliza kwa nini watu walipe kiingilio ili wawaone wasanii wa injili wakimtukuza Mungu, ulijibiwa kuwa hata wahubiri huchukua sadaka.

Kimsingi, kuifanya sanaa ya injili kuwa kama biashara nyingine yoyote ambayo lengo lake kuu ni faida ni kupotoka. Ni sawa na mchungaji kuwa na kipawa cha uponyaji kisha akatoza watu ada ilhali kipawa kapewa na Mungu.

Hivyi ndivyo vipawa hutoweka.

Ulimwengu wa sanaa ya injili nchini Kenya una msukosuko mkubwa unaohotaji sala na mfungo ili kutatuliwa; tusichoke kuwaombea wasanii wetu, nao wajitume kujirekebisha.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wito EAC itume wanajeshi zaidi kukabili waasi DRC

WANDERI KAMAU: CBC: Jopo litilie maanani kuwapunguzia...

T L