• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Nilikunywa glasi moja pekee ya chang’aa nikaishia kupoteza mkono wangu na familia nzima

Nilikunywa glasi moja pekee ya chang’aa nikaishia kupoteza mkono wangu na familia nzima

KASSIM ADINASI na LABAAN SHABAAN

KAMA angejua ziara yake kwenye kilabu cha chang’aa mnamo Disemba 29, 2022 ingemfanya kuwa ombaomba, angekaa nyumbani huko Kodiaga, Kaunti ndogo ya Gem Yala.  

Bw Derrick Opiyo na mke wake walienda kupiga glasi moja ya pombe ya kienyeji akiwa mzima, alirudi nyumbani bila mkono mmoja.

Baba huyu wa watoto watatu alikuwa na tabia ya kwenda kujivinjari na mke wake kilabuni baada ya siku yenye kazi ngumu.

Alipoingia kwenye baa, alikutana na wateja wa kawaida na baadaye saa mbili jioni, walikuwa tayari kuondoka.

Akiwa karibu kutoka, kaka yake mkubwa Sylvester Opiyo aliwasili.

“Alifika nikiwa tayari kuondoka. Nilikuwa nimetosheka na starehe na nilichotaka ni kurudi nyumbani na mke wangu,” Bw Derrick alisema katika mahojiano na Taifa Leo.

Kaka yake alimsihi aendelee kukaa na kuzidi kubugia kileo kabla ya kuondoka.

“Aliagiza pombe yake na yangu. Nikakataa, hata hivyo, alizidi kuniomba nikae kidogo,” alisimulia.

‘Mambo yalichemka’ alipokosa kushika glasi ya chang’aa alipokuwa anahudumiwa na ikaanguka sakafuni.

“Mhudumu alidhani niliangusha glasi na haikuwa hivyo. Glasi ilianguka na kumwaga pombe,” akasema.

Alipoona kilichojiri, kaka yake alipandwa na hasira na kumparamia kisha kumpiga bila kujali.

“Kaka yangu alihisi amekosewa heshima na kuanza kunipiga. Alichukua panga na kunishambulia. Alinikata vibaya sana kwenye kifundo cha mkono wa kulia. Jereha hilo lilikuwa baya sana na kusababisha mkono wangu kuning’nia,” akaeleza Bw Derrick.

Wapiga sherehe waliokuwa kwenye baa waliondoka na kumwacha akishambuliwa.

Baada ya tukio hilo, aliachwa kwenye bwawa la damu kaka yake mshambuliaji akiondoka.

Wasamaria wema walimsaidia na kumpeleka hospitalini alipolazwa kwa miezi kadhaa.

“Mkono wangu ulitibiwa lakini ukafa na siwezi kufanya chochote katika hali hii. Mimi ni  mpakaji rangi na mwashi mwenye tajiriba ya kukita paa. Siwezi kufanya tena kazi hizo ngumu na inanibidi kuwategemea wengine,” aliteta.

Maisha yake ya kijamii yamesambaratika na ndoa imevurugwa kwa kushindwa kulisha familia.

“Nilikuwa mlezi. Nilifanya kazi kwa bidii kuipa familia maisha bora. Kama unavyoona leo, mke wangu hayuko nyumbani na watoto wanaishi na jamaa. Inaniumiza sana,” aliongeza.

Sylvester alishtakiwa katika mahakama ya Siaya mbele ya Hakimu Benjamin Limo na kutupwa ndani miaka 10.

  • Tags

You can share this post!

Niponge Nisiponge? Joshua Kutuny amegewa mnofu na Ruto...

Kijana, 20, aondolewa kesi ya ubakaji baada ya kudhihirisha...

T L