• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
SHINA LA UHAI: Kipindi kigumu kwa walio na HIV na TB

SHINA LA UHAI: Kipindi kigumu kwa walio na HIV na TB

Na PAULINE ONGAJI

MARUFUKU ya kutosafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine yaliyotokana na maradhi ya Covid–19 yalimuathiri vibaya Bi Lynn, 23, kama watu wengine wanaoishi na virusi vya HIV.

Kwa mkazi huyu wa kitongoji duni cha Mathare, katika Kaunti ya Nairobi, ambaye wakati huo pia alikuwa anaugua kifua kikuu (TB), mambo yalikuwa mabaya hata zaidi hasa ikizingatiwa kwamba hana ajira.

“Kabla ya Covid-19 nilikuwa nafanya vibarua vya hapa na pale, lakini pindi ugonjwa huu ulipotokea fursa hizi za kazi zikatokomea. Nililazimika kufulia watu nguo ili kupata pesa za kununua chakula ili niweze kumeza dawa zangu za kupunguza makali ya HIV (ARVs).”

Kutokana na sababu kuwa alikuwa pia anaugua TB, maisha yake yalikuwa magumu hata zaidi.

“Ilikuwa vigumu kupata dawa zangu za TB kutokana na marufuku hiyo iliyofanya iwe changamoto kwenda hospitalini,” aeleza.

Aidha, asema kwamba wagonjwa wengi waliogopa kwenda hospitalini kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya corona.

“Hasa kwa sisi ambao kingamwili yetu tayari imeathirika, tulikuwa na wasiwasi wa kuhatarisha afya yetu,” aeleza.

Lakini Bi Lynn alikuwa mmoja wa waathiriwa wa virusi vya HIV waliobahatika kukamilisha matibabu ya TB licha ya changamoto zilizotokana na maradhi ya Covid-19.

Duniani kote asilimia nane ya watu wanaougua TB pia wana virusi vya HIV huku Afrika ikiongoza kwa idadi, ambapo katika baadhi ya mataifa ya Afrika Kusini, asilimia hii inapita 50. Duniani kote, takriban nusu ya watu wanaoishi na HIV wanaokumbwa na TB hutambuliwa na kutibiwa TB.

Kulingana na ripoti iliyotolewa majuma mawili yaliyopita na shirika la Stop TB Partnership, vifo vinavyotokana na TB miongoni mwa watu walio na virusi vya HIV viliongezeka kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2010.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu hizo, mwaka jana vifo vilivyosababishwa na TB miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya HIV vilifikia 214 000 ambapo kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2021. Mwaka 2020, vifo vilivyotokana na TB miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya HIV viliwakilisha asilimia 14 ya jumla ya vifo vilivyotokana na maradhi ya kifua kikuu.

Mwaka jana, Shirika la Afya Duniani WHO lilisema kwamba kukatizwa kwa matibabu ya kifua kikuu hasa kutokana na athari za Covid-19, kumerejesha nyuma maafikio ya vita dhidi ya TB. Takwimu zilizokusanywa mwaka jana na WHO kutoka mataifa 84, zilionyesha kwamba kulikuwa na upungufu wa takriban watu milioni 1.4, waliopokea matibabu ya TB mwaka wa 2020, ikilinganishwa na 2019. Upungufu huu ni wa 21%. Katika kikundi cha mataifa 10 yenye mzigo mkubwa wa TB, upungufu huu ulikuwa 28%.

Mapema mwaka huu, Dkt George Oballa, Mshauri wa Kiufundi – Idara ya udhibiti wa TB sugu, Mpango wa Kitaifa wa TB katika Wizara ya Afya alitabiri kwamba huenda mabadiliko ya huduma za matibabu ya TB kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 yakawa na athari kwa wanaougua kifua kikuu.

“Mabadiliko haya ni pamoja na viwango vya chini vya utambuzi wa TB, wahudumu wanaoshughulikia wagonjwa wa TB kuelekezwa katika sehemu zingine, kutozingatia masharti ya matibabu kutokana na hofu ya kuambukizwa maradhi ya TB, na vituo vya matibabu ya TB kubadilishwa na kuwa wodi za Covid-19,” alisema.

Duniani kote, maradhi ya TB ndio yanayoongoza kwa kusababisha vifo miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya HIV. Kabla ya 2020, vifo vilivyotokana na TB miongoni mwa watu walio na virusi vya HIV vilikuwa vinapungua. Mwaka wa 2020, mafanikio haya yalipinduliwa kutokana na maradhi ya COVID-19, na hivyo kuathiri ufikiaji wa huduma za utambuzi na matibabu ya TB.

“Kila siku takriban watu 600 wanaoishi na virusi vya HIV wanafariki kutokana na TB. Kwa sasa watu wanaoishi na virusi vya HIV wanakumbwa na mzigo mkubwa ambapo tishio lao sio tu kwa virusi vya HIV lakini pia maradhi ya COVID-19 na TB,” alisema Dkt Lucica Ditiu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Stop TB Partnership.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Stop TB Partnership, Dkt Lucica Ditiu. PICHA | MAKTABA

Kulingana na Dkt Lucica, licha ya kwamba kuna mbinu za kuzuia na kutibu TB, ufadhili wa TB unasalia chini ukilinganisha na maradhi mengine.

Ripoti mpya iliyozinduliwa siku chache zilizopita kwa jina Tuberculosis Research Funding Trends, 2005–2020, ilionyesha kwamba mwaka 2020, ufadhili wa TB ulifikia US$915 milioni. Kiwango hiki ni chini ya nusu ya pesa ambazo mataifa yaliyoshiriki katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa miaka mitatu iliyopita, yaliamua zitengewe matibabu ya maradhi haya. Makubaliano yao yalikuwa kwamba US$2 bilioni zitengewe matibabu ya TB.

Huku ufadhili wa huduma za matibabu ya TB ukiwa umepunguzwa,, wataalam wanaonya kwamba tujiandae kushuhudia ongezeko la idadi ya vifo kutokana na TB miongoni mwa wagonjwa walio na virusi vya HIV katika kipindi cha miaka ijayo.

Kulingana na Dkt Lucica, ili kukabiliana na janga hili uwekezaji zaidi, vifaa vya kisasa vya kutambua kifua kikuu, uchunguzi wa kila mara wa maradhi haya (kama vile X-ray na rapid molecular tests) utahitajika.

“Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila mmoja kila mahali pasipo ubaguzi wowote ule, anafikia huduma muafaka za utambuzi na matibabu ya maradhi haya,” aliongeza Dkt Ditiu.

You can share this post!

‘Taste of Nairobi’ yatoa fursa ya kipekee...

STEVE ITELA: Uhifadhi wa mazingira si hatia na wanaharakati...

T L