• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
BAHARI YA MAPENZI: Usaliti wa mapenzi katika ndoa

BAHARI YA MAPENZI: Usaliti wa mapenzi katika ndoa

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

KATIKA maisha ya mapenzi, hakuna kitu kibaya kama kujeruhi hisia za mtu anayekupenda.

Usaliti ni sumu namba moja ya mapenzi ya kweli.

Na maumivu ya kusalitiwa hakuna awezaye kuyaeleza yakaeleweka. Maumivu ya kutendwa katika mapenzi ni rahisi sana kuubadilisha moyo wa upendo kuwa moyo wa chuki.

Mara nyingi unapotokea usaliti katika ndoa, swali kubwa kwa aliyesalitiwa ni amekosea wapi ama ametenda nini hadi mwenzake amsaliti. Hapa unaweza kusikia aliyesalitiwa akisema; “najitahidi kumfanyia mambo mengi mazuri, bado anaonekana haridhiki”.

Lakini je, ukweli ukoje? Kukwazana ni mambo ya kawaida katika mapenzi na siku zote furaha ya mtu ni jukumu lake binafsi na wala sio la mtu mwingine. Hivyo hatua ya kwanza na muhimu unapokuwa katika uhusiano ni kuondoa dhana kwamba unalo jukumu la kuhakikisha mwenzako ana furaha wakati wote.

Jambo muhimu katika ndoa ni kuhakikisha kunakuwa na nafasi ya wanandoa kujadili hali ya ndoa yao. Hii ni sawa na ilivyo katika biashara kwamba wafanyabiashara wakati fulani hujadili hali ya maendeleo ya biashara ili kujua kama kuna matatizo na jinsi ya kuyatatua.

Nimewahi kuzungumza na watu wanaosaliti ndoa. Baadhi yao ninapowauliza wanaonaje watoke kwenye ndoa na kuoana na hao wa nje, jibu huwa hawawezi kwa sababu wanasaliti si kwa sababu hawana mapenzi na wake ama waume zao, bali wakati mwingine ni kutofautiana, kuzozana ama kulipiza kisasi.

Sababu inayoongoza kwa wanandoa kusababisha usaliti ni kukosa tendo la ndoa, kwa mfano wakati kwa wanaume tendo la ndoa ni muhimu sana, furaha ya wanawake walio wengi sio kwenye tendo hili, bali uhakika wa kupatikana kwa mahitaji ya ndani na amani.

Wengine hawapati mapenzi ya kweli kwa sababu tu mke au mume hamjali, kitendo ambacho kinasababisha baadhi yao kuona kwamba suluhu pekee ni kwenda nje ya ndoa.

Halafu wapo wale wanaojisahau baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu. Hapa unakuta mwanamke hajali tena kumvutia mumewe kwa mavazi, mwonekano na mambo mengine yanayoleta raha ya macho.

Halikadhalika mume naye hajali tena usafi ama kuwa na mwonekano ambao utamvutia mkewe, kiasi kwamba wengine hata kuoga inakuwa ni shughuli.

Hizi ni sababu lakini hazilahalalishi usaliti wa jinsi yoyote kwa wanandoa ama wapenzi.

Kwani suluhisho ya yote hayo lipo kwenye mazungumzo na kuwa wazi kwa mwenzako bila kuficha.

Iwapo kunakuwa na mazungumzo ya mara kwa mara kwa wanandoa, kunakuwa pia na nafasi ya kupata suluhu ama kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza baina yao.

Na pale unapoamua kufanya usaliti kwa mwenzako, utambue kwamba usaliti hauna siri. Bali yule uliye naye anakuvumilia akiamini atakubadilisha au utabadilika.

Na muhimu katika yote, usimuache uliyempenda kwa uliyemtamani. Mali na pesa ni vitu vya kupita bali penzi la ukweli hudumu, kwani linaweza kuishi bila mali na pesa.

[email protected] 

HAKUNA kitu kinachoumiza mtu kama kugundua kwamba mpenzi wake anayemwamini kwa dhati huwa anamsaliti.

Usaliti huu unaweza kuwa mmoja wa wanandoa kuwa na mipango ya kando au kushiriki mapenzi na mtu mwingine mara moja tu. Unaweza pia kuwa kuvunja ahadi na viapo vya ndoa au kuanika siri za ndoa au za mpenzi wako kwa watu wengine. Hata hivyo, usaliti ambao umekuwa ukisambaratisha ndoa na hata kuzua maafa ni uzinifu.

Anayeshiriki tabia hii hatarajii mchumba wake kufurahi akigundua. Ni tabia ambayo bila shaka imechangia mahusiano mengi ya mapenzi na ndoa kuvunjika ghafla na kwa kishindo. Sio wengi wanaovumilia watu ambao wanawasaliti licha ya kuapa kuwa waaminifu kwao na kuwapenda kwa kila hali. Imesemwa na ninaamini kwamba usaliti mkubwa ambao mtu anaweza kumtendea mume au mpenzi wake, ni kugawa pembeni.

Hakuna anayeweza kuvumilia akigundua kwamba mume au mke wake anaanika uchi wake kwa mtu mwingine. Haya ni makosa ambayo yametajwa katika Maandiko Matakatifu na sheria za nchi kama mojawapo ya sababu za talaka. Mtu akigundua kwamba mwenzake anazini, iwe kwa kuwa na kimada, mpango wa kando au sponsa, huwa anahisi amedharauliwa hasa ikiwa amewekeza nguvu, rasilmali, wakati na hisia zake kwa anayemsaliti.

Anayesalitiwa huwa anaandamwa na mkururo wa mawazo kujaribu kung’amua sababu ya mume au mke wake kumfanyia hivyo.Katika kutafuta kiini, wengi huwa wanatumbukia katika mfadhaiko na maisha yao kuvurugika. Kuna wanaoshindwa kujizuia na kuchukua sheria mikononi au pia kulipiza kisasi na kwa kufanya hivyo kuharibu ndoa kabisa huku wakiweka maisha yao kwenye hatari zaidi.

Ninasema hatari zaidi kwa sababu anayeanza tabia ya usaliti tayari huwa amehatarisha maisha yake na ya mchumba wake. Hii ni kwa sababu anaweza kupata maradhi na kumuambukiza mwenziwe. Visa vimeripotiwa vya jinsi usaliti wa mapenzi unavyosababisha maafa ikiwa ni pamoja na mauaji.

Jambo lililo wazi ni kwamba anayekusaliti kwa hali yoyote ile, hakuthamini na hakutakii mema. Japo ni jambo lenye uchungu mwingi, sidhani linafaa kusababisha mtu kuumia au kuua kwa sababu ya mtu asiyemdhamini. Binafsi ninaamini hatua ya busara ni kujitengana na mtu kama huyo ili kuokoa maisha yako. Hakuna makosa kujitenga na mume au mke anayehatarisha maisha yako kwa kusambaza mwili wake kwa mtu.

Mara nyingi, wanaosaliti wachumba wao kwa kuzini huwa hawana sababu ya kufanya hivyo. Hii haimaanishi kwamba hakuna sababu zinazoweza kusukuma mtu kutoka nje ya ndoa yake. Hata hivyo, kwa mtu anayeheshimu taasisi ya ndoa, atatumia hekima kusuluhisha suala lolote linaloweza kumfanya ashawishike kusaliti mke au mume wake.

Tutakuwa tukijidaganya kusema hakuna kinachoweza kushawishi mtu kusaliti mchumba wake. Vishawishi ni vingi na vitaendelea kuzuka. Kinachohitajika ni kudumisha heshima ya mtu binafsi na kukwepa vishawishi hivyo.

[email protected]

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Kuwakinga wasichana matineja mtandaoni

Arsenal wacharaza Leicester na kurejea ndani ya mduara wa...

T L