• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Arsenal wacharaza Leicester na kurejea ndani ya mduara wa nne-bora EPL

Arsenal wacharaza Leicester na kurejea ndani ya mduara wa nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL walidumisha uhai wa matumaini ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao kwa kupepeta Leicester City 2-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Machi 13, 2022 ugani Emirates.

Ushindi huo uliwarejesha vijana hao wa kocha Mikel Arteta katika nafasi ya nne kwenye jedwali la EPL na sasa wanajivunia alama 51, moja zaidi kuliko nambari tano Manchester United. Nafuu zaidi kwa Arsenal ni kwamba wana michuano mitatu zaidi ya kusakata ili kufikia idadi ya mechi 29 ambazo tayari zimepigwa na Man-United ligini msimu huu.

West Ham United (alama 48), Wolves (46) na Tottenham Hotspur (45) ni vikosi vingine vinavyopigania nafasi ndani ya mduara wa nne-bora.

Thomas Partey alifungulia Arsenal ukurasa wa mabao katika dakika ya 11 baada ya kushirikiana vilivyo na fowadi Gabriel Martinelli.

Partey ambaye ni raia wa Ghana angalifunga bao jingine katika kipindi cha pili ila kombora lake likabusu mwamba wa goli la Leicester ambao sasa wanakamata nafasi ya 12 kwa alama 33 sawa na Crystal Palace na Brighton.

Bao la pili la Arsenal lilifungwa na nahodha Alexandre Lacazette katika dakika ya 59 baada ya beki Caglar Soyuncu wa Leicester kunawa mpira ndani ya kijisanduku.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Usaliti wa mapenzi katika ndoa

Mashabiki wazomea Neymar na Messi kwa kutotambisha PSG...

T L