• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
GWIJI WA WIKI: Mwimbaji Sam Mpole

GWIJI WA WIKI: Mwimbaji Sam Mpole

Na CHRIS ADUNGO

WASANII waimbao kwa Kiswahili wamekuwa wakitia fora katika tasnia ya muziki ambayo hutegemea zaidi ujuzi wa kusuka, kusana na kuremba maneno.

Ingawa muziki wa Bongo Flava ni maarufu sana miongoni mwa wasanii wa Tanzania, wapo Wakenya wanaozidi kuinukia vyema katika fani hii. Upekee wao umejikita katika upevu wa masimulizi, ukwasi wa msamiati, ujuzi wa kufumbata ujumbe na umahiri wa kukisarifu Kiswahili.

Miongoni mwa waimbaji hao ni Samuel Karani almaarufu Sam Mpole ambaye hachoki kusoma vitabu katika juhudi za kujifunza maneno rahisi na matamu ya kuvutia kabla ya kufinyanga muziki wa kutamananisha.

Sam alizaliwa mnamo 1994 katika kijiji cha Kiathi, Kaunti ya Tharaka Nithi. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto wanne wa Bi Stephenina Muthoni na Bw Charles Ntwiga.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Mutiiguru (2001-2008) kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Itara (2009-2012). Shule hizi zinapatikana katika eneo la Muthambi, Marima, Tharaka Nithi.

Alifanya vibarua vya kuuza maziwa na kuchuuza laini za simu jijini Nairobi kabla ya kujiunga na chuo cha Kenya Institute of Professional Studies (KIPS) kusomea Mawasiliano ya Umma mnamo 2015.

Alifuzu 2017 baada ya kutoa wimbo wake wa kwanza ‘Mama’ mnamo Mei 2016. Alirejea makwao Tharaka Nithi kuwa ‘fundi wa mkono’ katika maeneo mbalimbali ya ujenzi.

Ingawa Sam alitamani kuwa mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano tangu utotoni, uanamuziki ulimteka akiwa mwanafunzi wa darasa la 7.

Walimu waliotambua kipaji chake walimhimiza ajiunge na bendi ya shule na wakawa wepesi kumjumuisha katika makundi ya kutumbuiza wageni kwa nyimbo na mashairi katika hafla muhimu.

“Niliwakilisha shule yangu ya msingi katika mashindano mengi ya kutunga na kukariri mashairi. Kuwasilisha mbele ya hadhira kulinipa ujasiri. Insha nzuri nilizoziandika zilinizolea tuzo za haiba kutoka kwa walimu na kunifanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzangu,” anasema.

Mnamo 2018, Sam alikutana na prodyusa Dully Catch aliyemsaidia kurekodi nyimbo 20 jijini Nairobi. Alifyatua video ‘Wataisoma’ miaka miwili baadaye na kazi hiyo ikamchochea kuhamia Mombasa mnamo Julai 2021 kwa lengo la kujikuza zaidi kisanaa katika mazingira ya Uswahilini.

Kibao kilichomkweza kimuziki na kumzolea sifa tele katika mtindo wa Bongo Flava ni ‘Kidedea’ alichokitoa Disemba 2021. Video yake ya hivi karibuni zaidi ni ‘Elewa’ aliyoiachilia wiki hii. Kufikia sasa, Sam anajivunia vibao 26 anavyovitumia kuipa jamii mwelekeo na kupigia chapuo makuzi ya Kiswahili.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kushirikiana kikazi na wasanii Otile Brown, Nadia Mukami, Jovial, Mejja na Khaligraph Jones.

Sam anaistahi sana familia yake. Ana mke Moreen Kibara na mtoto Delaney Kawira.

You can share this post!

Wavinya Ndeti ajiuzulu kazi serikalini kuwinda kiti cha...

Tergat kushughulikia nidhamu Olimpiki ya msimu wa baridi...

T L