• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
HUKU USWAHILINI: Ugomvi nyumbani ni burudani mtaa mzima

HUKU USWAHILINI: Ugomvi nyumbani ni burudani mtaa mzima

NA SIZARINA HAMISI

IWAPO unaishi Uswahilini bila shaka umeshakutana na kunguru weusi.

Wale kunguru ambao wamekithiri kwa wizi kama vile wamesomea kazi hiyo.

Ukiweka mboga yako jikoni na usifunike vyema, ndege hawa wana utaalam wa kung’ofoa nyama ya moto ikiwa inatokota jikoni, kama hiyo haitoshi, ukisahau uache mlango wazi, sio ajabu kupata wameingia ndani na kunyakua chochote ambacho kinaweza kuwaondolea njaa yao. Kwa kifupi, huku kwetu huwa tunawaita ndege watu.

Kwamba hata unapowafukuza, unaweza kupata mnaangaliana, huwa hawashtuki wala kuogopa watu.

Ukigeuka upande mwingine usishangae kukutana na majirani katika vyumba vya kupanga wanaoshindana kwa milio ya redio mchana na miguno ya kuchangamsha mwili usiku.

Ukipita mchana kwenye maeneo haya usistaajabu kupata milio ya miziki ikishindana kwa sauti kutoka nyumba moja hadi nyingine na ndani yake unapata mchangayiko wa ladha mbalimbali za muziki kuanzia taarab, midundo ya taratibu, ngoma za asili ya Kenya na hata miziki ya kuruka majoka.

Ukisema ukatishe mtaa mwingine ni kawaida kukuta wanaume watu wazima, tena walioshiba vizuri wakiwa wamekaa kijiweni mchana kutwa wakicheza bao na kubishana siasa ama pia wakiangalia wapita njia na kuanzisha majadiliano kwa kadiri mtu anavyopita.

Usije kuuliza hawa wanaume wanafanya kazi muda gani na huko nyumbani kwao wanakidhi vipi mahitaji ya familia. Hawa wanaume huwa ni watata na wakorofi kupitiliza na mara nyingi hata wake zao huwa ni chakula ya wajanja wa huku kwetu wanaojua kutafuta na kusaka maisha kwa bidii.

Huku kwetu ukitokea ugomvi chumbani kwa wanandoa huwa ni burudani kwa majirani. Kwani watu huitana na kutega masikio ikibidi hadi dirishani kusikiliza sokomoko inayoendelea humo ndani.

Na kesho yake usishangae unapopita mtaani, huku vijiweni watu wakiongea kwa mafumbo jinsi mtu alivyodundwa kama mpira wa kona na wengine wanaweza kuthubutu hata kurudia yale maneno mliyokuwa mnatupiana wakati mnagombana.

Yaani huku kwetu ugomvi wa jirani ni burudani ya mtaa mzima.

Huku kwetu suala la ustaarabu ni kama kumpigia mbuzi gitaa na matarumbeta aweze kuucheza muziki. Kwamba tabia zetu tunazijua wenyewe na suala la ustaarabu linategemea siku na wakati, ingawa muda mwingi tunaishi kwa mazingira yaliyopo.

Ni kawaida kupata mtoto wa jirani kachuchumaa pembeni ya nyumba akijiachia shughuli asili za mwili na wakati mwingine hata wale wanaume wanaopita usiku wakiimba mtaani baada ya kunywa pombe za kienyeji, huacha michirizi ya haja zao pembezoni kwa nyumba.

Haya ndio maisha yetu, na wenyewe tumeyazoea.

[email protected]

You can share this post!

JUKWAA WAZI: Wandayi na Kamande watofautiana vikali kuhusu...

London Marathon: Yehaulaw avunja utawala wa Kenya wa miaka...

T L