• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Gumo: Alikuwa akikohoa wapinzani wanachemua

Gumo: Alikuwa akikohoa wapinzani wanachemua

KWA HISANI YA KYB

KWA watu wengi, Fredrick Fidelis Gumo, au Fred Gumo anavyofahamika zaidi, ni upanga unaokata kuwili.

Aina ya mtu anayechukiwa na kupendwa kwa wakati mmoja.

Kama yuko upande wako, anaweza kuwa muhimu na hatari pia.

Hachelei kupigana akikosewa na ni mchangamfu sana mambo yakimwendea vizuri.

Wakati wa enzi zake katika siasa, Gumo alihusishwa na kauli mbili za Kiswahili – Jeshi la Mzee na Kaa Ngumu.

‘Jeshi la Mzee’, au Jeshi la Daniel arap Moi, lilikuwa kundi hatari ambalo Gumo aliongoza akiwa mbunge wa Westlands katika kaunti ya Nairobi, ambalo lingefanya chochote kulinda maslahi ya Moi na ya chama tawala cha KANU katika jiji kuu la Kenya.

‘Kaa Ngumu’ ilikuwa kauli mbiu ya Gumo miaka yake ya mwisho katika siasa.

Si ajabu kwamba aliwakilisha eneobunge la Westlands kwa takriban miaka 20 (1994 hadi 2013).

Gumo alikuwa akitumia kauli mbiu ya ‘kaa ngumu’ kuhimiza wanasiasa wengine kupigania maslahi yao na watu wakaanza kutumia kauli, ‘kaa ngumu kama Gumo’.

Kauli hii inamrejelea kwa mukhutasari mtu aliyeanza kama karani hadi akawa waziri katika serikali lakini aliyekuwa akipata washirika wanaofaa kwa wakati unaofaa.

Alisukuma maslahi yake katika serikali na katika siasa na alikuwa mtu mtulivu alipohitajika kuwa hivyo, kama mnamo 2013, alipoteuliwa waziri wa Ustawi wa Ukanda na akaanza kuchukulia majukumu hayo rasmi.

Kinyume na walivyotarajia wengi, Gumo alitekeleza majukumu yake kwa ufanisi akiwa waziri wa Ustawi wa Kanda na hata baadaye alipopewa jukumu la kusimamia Wizara ya Serikali za Mikoa kama kaimu.

Huu ulikuwa wakati Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi alipojiuzulu kuzingatia kampeni zake za urais.

Katika Wizara ya Serikali za Mikoa, waziri msaidizi alikuwa Robinson Githae na Katibu wa wizara alikuwa Samuel Kirui.

Maisha ya kisiasa ya Gumo yalikuwa na ubishi kila wakati.

Aliteuliwa Meya wa Kitale, wilaya ya Trans Nzoia (sasa kaunti ya Trans Nzoia) mwaka wa 1974 akiwa na umri wa miaka 27 na akahudumu katika wadhifa huo kwa miaka sita.

Alijiuzulu kujiunga na siasa za ubunge mwaka wa 1979 na hata akamshinda mwanasiasa mashuhuri Masinde Muliro, katika uchaguzi uliojawa na madai ya wizi wa kura.

Gumo alianza kuibuka katika siasa za Kenya.

Mnamo 1984 Mahakama Kuu iliamua kuwa ushindi wake dhidi ya Muliro kwenye uchaguzi wa 1983 katika eneobunge la Kitale Mashariki ulikumbwa na udanganyifu mkubwa.

Gumo hakugombea uchaguzi mdogo uliofuatia.

Alijaribu kugombea kiti cha eneobunge la Kwanza kwenye uchaguzi mkuu wa 1988 lakini akashindwa na Noah Wekesa.

Mwaka wa 1989, aliteuliwa mwenyekiti wa Nairobi City Commission, uteuzi wa kwanza na Afisi ya Rais kwa kuwa teuzi za awali zilikuwa zimefanywa na Waziri wa Serikali za Mikoa.

Utashi wa siasa wa Gumo ulikuwa ukipata nguvu na mnamo 1992, mwana wa kwanza wa Pius Gumo na Martina Gumo alihamishia kambi yake ya kisiasa hadi nyumbani kwake asili, Bunyala, katika wilaya ya Busia (sasa kaunti ya Busia), lakini alibwagwa na James Osogo kwenye mchujo.

Miaka minne baadaye, aligombea kiti cha ubunge cha Westlands kwenye uchaguzi mdogo baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Amin Walji.

Baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa 1997 akiwa mbunge wa pekee wa Kanu katika Nairobi, Rais Moi alimzawadi kwa kumteua waziri msaidizi.

Mnamo Aprili 14, 2008, Gumo aliteuliwa waziri kamili wa Ustawi wa Ukanda katika serikali ya Rais Mwai Kibaki.

You can share this post!

SOKOMOKO WIKI HII: Kisiasa Savula ni Mudavadi kimwili...

Beki wa zamani wa Man-United kutegemewa na Gambia kwenye...

T L