• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
EPL: Chelsea yapiga Spurs kwa mara ya tatu chini ya wiki tatu

EPL: Chelsea yapiga Spurs kwa mara ya tatu chini ya wiki tatu

Na MASHIRIKA

MABAO mawili katika kipindi cha pili yalisaidia Chelsea kucharaza Tottenham Hotspur kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha wiki tatu.

Hakim Ziyech alifungulia Chelsea ukurasa wa mabao katika dakika ya 47 baada ya kushirikiana vilivyo na Callum Hudson-Odoi. Bao la pili lilijazwa kimiani na beki Thiago Silva aliyekamilisha krosi ya Mason Mount katika dakika ya 55.

Chelsea walivuna ushindi huo baada ya kuzamisha Spurs kwenye michuano ya mikondo miwili ya nusu-fainali ya Carabao Cup kwa jumla ya mabao 3-0 na kujikatika tiketi itakayowakutanisha na Liverpool kwenye fainali.

Kichapo kutoka kwa Chelsea kilikuwa cha kwanza kwa Spurs kupokezwa ligini tangu kocha Antonio Conte aaminiwe fursa ya kuwa mrithi wa Nuno Espirito Santo mnamo Novemba 2021. Conte ambaye pia amewahi kunoa Juventus, Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, aliwahi kuongoza Chelsea kunyanyua taji la EPL na Kombe la FA mnamo 2016-17 na 2017-18 mtawalia.

Chelsea walikuwa kileleni mwa jedwali la EPL mnamo Disemba 1, 2021 baada ya kukomoa Watford 1-0. Hata hivyo, walianza kusuasua na wakajizolea alama 11 pekee kutokana na mechi tisa zilizofuata. Matokeo hayo yalididimiza matumaini yao ya kufukuzana na Manchester City wanaopigiwa upatu wa kuhifadhi ufalme wa EPL.

Chelsea kwa sasa wanakamata nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 10 nyuma ya Man-City wanaoselelea kileleni kwa pointi 57. Liverpool waliotandika Crystal Palace 3-1 ugani Selhurst Park wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 48 huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na Arsenal walioambulia sare tasa dhidi ya Burnley uwanjani Emirates.

Spurs wanakamata nafasi ya saba kwa alama 36 sawa na Arsenal. Nafuu zaidi kwa Spurs ni kwamba wana mechi tatu zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano 23 ambayo imetandazwa na Chelsea ligini.

Chelsea hawatanogesha mchuano wowote wa EPL hadi Februari 19 kwa kuwa wataanza kushiriki Kombe la Dunia kwa Klabu baada ya kutawazwa wafalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwishoni mwa 2020-21.

Chelsea walishuka dimbani wakiwa na ulazima wa kushinda Spurs ili kuendeleza presha kwa Man-City Liverpool na kuweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora.

Matumaini ya Chelsea ya kutia kapuni taji la EPL muhula huu yalididimia zaidi katika kipindi cha wiki chache zilizopita baada ya kushinda pambano moja pekee kati ya nane. Isitoshe, masogora hao wa kocha Thomas Tuchel wamejizolea alama sita pekee kutokana na mechi tano zilizopita ligini.

Chelsea sasa wameshinda mechi zote nne zilizopita dhidi ya Spurs katika mapambano yote, ukiwemo ushindi wa 3-0 katika EPL ugenini mnamo Septemba 2021. Spurs hawajawahi kuangusha Chelsea ligini tangu Novemba 2018.

Spurs walishuka dimbani wakiwa na motisha ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-2 dhidi ya Leicester ligini mnamo Januari 19, 2022 ugani King Power.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Arsenal 0-0 Burnley

Crystal Palace 1-3 Liverpool

Leicester 1-1 Brighton

Chelsea 2-0 Tottenham

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuoka mkate mtamu wa siagi

TALANTA YANGU: Yvonne ni Lupita anayeinukia

T L