• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
MALEZI KIDIJITALI: Teknolojia yavutia wanaume kwa malezi

MALEZI KIDIJITALI: Teknolojia yavutia wanaume kwa malezi

INGAWA ina changamoto zake ikizingatiwa kuwa inabadilika kila wakati na kwa haraka, teknolojia imerahisisha ulezi wa watoto hasa kwa wanaume.

Wataalamu wanasema kwamba tafiti mbali mbali zinaonyesha kuwa wazazi wa umri mdogo wanakiri kwamba teknolojia imekuwa nguzo ya malezi huku wakiendelea na shughuli zao za kila siku mbali na nyumbani.

Hasa wanasema kwamba kwa sababu ya uvumbuzi wa teknolojia, wanaume wanaweza kufuatilia malezi na tabia za watoto wao iwe ni kupitia kamera au simu za mkono.

Kulingana na mtaalamu wa malezi dijitali Agnes Sudi, wazazi wanaume wa kizazi kipya wanakumbatia teknolojia wakisema inawafanya wapate habari zaidi na ushauri kuhusu malezi kuliko ilivyokuwa miaka ya zamani.

“Tafiti zinaonyesha kuwa wazazi wa milenia wanaamini kwamba kupitia tekinolojia wanaweza kupata habari na ushauri kuhusu malezi kwa urahisi wakiwa popote pale. Wanaweza pia kutumia vifaabebe kufuatilia tabia na malezi ya watoto wao,” asema Sudi.

Kulingana na utafiti wa Pew Research mwaka 2021, asilimia 30 ya wazazi wanasema mabadiliko ya teknolojia yameimarisha elimu na burudani kwa watoto na kufanya kazi yao ya ulezi kuwa rahisi na ya kufurahia.

“Kwa sababu ya tekinolojia, watoto wanaweza kucheza michezo kwa burudani au elimu. Wanapofanya hivi, mzazi anapata nafasi ya kufanya kazi za nyumbani bila kutatizika,” unaeleza utafiti huo.

Sudi anasema kwamba tekinolojia pia imefanya watoto kuwa werevu sana na inawawezesha kusoma kwa haraka.

Anasema kwa sababu ya tekinolojia wazazi wanaweza kupata habari na huduma za kisaikolojia kukabiliana na changamoto za malezi na pia kujifunza jinsi ya kufanya mtoto kuwa bora zaidi.

“Mtandao unasaidia zaidi kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu jinsi ya kusaidia mtoto kujijenga kisaikolojia miongoni mwa mambo mengine muhimu ya malezi,” asema.

Utafiti wa Pew Research pia ulisema kuwa kwa sababu ya teknolojia wanaume wengi wanahusika na malezi ya watoto wao kuliko ilivyokuwa awali.

You can share this post!

Rais apoteza washirika wake wakuu kwa Ruto

Joho avunja kimya cha muda mrefu na kurai madkatari wasigome

T L