• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
MITAMBO: Rain gun inatumia jua kuinyunyizia mimea yako maji

MITAMBO: Rain gun inatumia jua kuinyunyizia mimea yako maji

NA RICHARD MAOSI

SIKU za nyuma wakulima walikuwa wakitegemea kuajiri vibarua, kukodisha punda au kuteka maji kutoka kwenye mito ya misimu ili kunyunyizia mimea yao maji.

Mwisho wake ulikuwa ni kutumia gharama nyingi na kupoteza muda wa kuyafikisha maji shambani.

Hii ni kwa sababu moja ya tatizo kubwa katika biashara ya kilimo ni ukosefu wa nishati nafuu ambayo inaweza kutumika katika shughuli ya kunyunyizia mimea maji.

Hata hivyo ujuzi wa teknolojia na sayansi umekuja na mbinu nyingine mwafaka ya kutumia, ikizingatiwa kuwa kuna mengi ya kuchagua mkulima anapochagua mtambo au mtindo wa kufikisha maji shambani.

“Teknolojia yenyewe ambayo inafahamika kama sunculture ni nafuu na inaweza kumfaa mkulima anayeendesha kilimo cha aina yoyote endapo analenga kutengeneza faida katika kilimo,” asema Erastus Matete aliye mtaalam wa unyunyuziaji kutoka Grekkon Limited.

Matete amekuwa akiwasaidia wakulima sio tu kuendesha kilimo sahihi bali pia kuwahimiza namna ya kutumia kawi safi ya miale ya jua, hususan karne hii wakati ambapo kiwango cha mvua kinazidi kudidimia kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Erastus Matete akionyesha matumizi ya mtambo wa rain gun, teknolojia inayotumika kunyunyizia mimea maji. PICHA | RICHARD MAOSI

Anaamini kuwa mbinu hii itawasaidia wakulima wadogo mashinani wenye kipato kidogo ambao bado hawajafikiwa na umeme.

Aidha, wakulima wanaoendesha kilimo katika kipande kikubwa cha ardhi wanaweza kufaidika na mbinu hii ili kukwepa gharama kubwa ya kulipia umeme wa stima au kununua jenereta ya petroli ama dizeli.

Mtambo wa Solar Rain gun Huu ni uvumbuzi wa mtambo mdogo unaotumia miale ya jua kunyunyizia mimea maji, hasa kwa wakulima wadogo ambao hawana hela za kutosha kununua mitambo husika.

Matete anasema mtambo mdogo wa rain gun unaweza kunyunyiza maji katika kipande cha ardhi cha robo ekari kwa mzunguko mmoja tu, vilevile mtambo mkubwa unaweza kunyunyiza maji katika ekari moja kwa mzungungo mmoja.

Hii ikimaanisha kuwa chini ya dakika 30 eneo lote huwa limejaa unyevu.

Ikumbukwe kuwa mtambo wa rain gun sprayer ambao ndio hutumika kunyunyizia shamba una uwezo wa kuyarusha maji kwa shinikizo kubwa kiasi kwamba humchukua mkulima chini ya nusu saa kunyunyizia robo ekari.

Isitoshe, miale ya jua ndiyo huelekeza umeme katika pampu ambayo hatimaye huyavuta maji kutoka kwenye kisima au chemichemi ya mto na kuyasafirisha shambani.

Anawashauri wakulima kutumia kifaa hiki kunyunyizia mimea yao maji, hususan endapo wanatokea katika sehemu ambazo fangasi huathiri mavuno.

Alifichulia Akilimali kuwa kwa sababu ya shinikizo kubwa ya kurusha maji mtambo wenyewe hauwezi ukatengeneza nyufa ya kupitiza michirizi ya maji kwani imetengenezwa na chuma dhabiti aina ya steel.

“Kifaa chenyewe kitawafaa wakulima wa mboga aina ya kabeji, sukumawiki na spinachi ambao wanalenga kuyauza mazao yao katika soko la nje,” asema kwani mimea yenyewe huhitaji kiwango kikubwa cha maji.

Kifaa chenyewe hakiwezi kuyaharibu maji, kinyume na aina nyinginezo ya vifaa ambavyo huyafanya maji yakavuja na kutapakaa ardhini.

Mkulima atahitaji vyanzo vya maji ya kutosha kama vile mito au vidimbwi ili kuyapata matokeo mazuri kwa kuutumia mtambo wenyewe.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Juhudi za kutema ukuzaji tumbaku zaanza kufaulu

UJASIRIAMALI: Pikniki zake ni za kupigiwa mfano mijini

T L