• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
ZARAA: Juhudi za kutema ukuzaji tumbaku zaanza kufaulu

ZARAA: Juhudi za kutema ukuzaji tumbaku zaanza kufaulu

NA LABAAN SHABAAN

UTAFITI unadhihirisha maelfu ya wakulima Kenya hukuza tumbaku kwa sababu tatu kuu; mtazamo wa faida kubwa, ugumu wa kupata mkopo wa pembejeo wa zaraa nyingine na kuwa ni njia ya kuchuma fedha kumudu gharama za maisha.

China, Brazil na India ni nchi zinazozalisha tumbaku nyingi duniani huku Zimbabwe, Zambia na Tanzania zikiwa baadhi ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji Afrika. Hii ni kulingana na Ripoti ya 2020 ya Shirika la Takwimu la Ujerumani, Statista.

Mamia ya wakulima katika Kaunti ya Migori wanatarajiwa kutema kilimo cha tumbaku na kuzamia mimea mingine endelevu kupitia mradi wa mashamba bila tumbaku kwa kimombo “Tobacco Free Farms (TFF)” uliozinduliwa Machi 2022.

TFF ni mpango shirikishi wa Serikali ya Kenya, Shirika la Afya Duniani (WHO), Programu ya Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO).

Wakulima wa Migori wanakuza maharagwe yenye madini ya chuma ya kiwango cha juu (high iron beans) (HIB) kuwa zao mbadala.

Kwa mujibu wa WFP, mwaka wa 2021 shirika hilo lilinunua tani 134 za maharagwe kutoka kwa wakulima waliohama kilimo cha tumbaku.

“Kufikia wakati wa uzinduzi wa kwanza wa mradi huu Migori ilikuwa tayari imevuna tani 200 za maharagwe kwenye mashamba ekari 370 yanayosimamiwa na wakulima 330 waliotema tumbaku,” alisema Katibu wa Kaunti Christopher Rusana.

Mashirika yanawasaidia kwa mafunzo, pembejeo ya thamani kama mbegu na mbolea, na soko tayari kwa mazao kupitia mpango wa ununuzi wa WFP.

Asasi hizi zinaamini msaada huu kwa wakulima utawafanya wakulima waache ukuzaji tumbaku kimkataba na kukumbatia kilimo mbadala ambacho kitasaidia kulisha jamii badala ya kudhuru afya wakidhani kutakuwa na soko la muda mrefu.

John Meng’anyi ni mmoja wa wakulima walioambaa kilimo cha tumbaku na kuanza kupanda HIB kama vile rosecoco katika shamba la ekari 2 eneobunge la Kuria Magharibi Kaunti ya Migori.

“Tofauti na tumbaku inayokomaa baada ya miezi tisa, maharagwe hukomaa ndani ya miezi mitatu hivyo basi inanizidishia faida,” Meng’anyi anaambia Akilimali.“Shamba langu linanivunia zaidi ya magunia 15 ya 90kg kwa msimu ninayoyauza kwa Sh8,000 kwa gunia,” anaongeza.

Meng’anyi anaepuka madhara ya ukuzaji tumbaku kama vile uchafuzi wa mazingira, uhusishaji wa watoto katika kilimo, athari za kiafya na ufinyu wa utoshelevu wa chakula kwa kutokuza vyakula shambani.

Ripoti ya Jiografia ya Kiuchumi ya Wakulima wa Tumbaku inafichua wakulima wa tumbaku wanatumia watoto kufanya kazi shambani kwa sababu ya kutamaushwa na gharama – bei ya chini ya mazao ya tumbaku huwazuia kumudu kulipa wafanyakazi wazoefu.

Majani ya tumbaku. PICHA | LABAAN SHABAAN

Michael Mitende ni mkulima wa tumbaku tangu 1984 Wadi ya Kakrao eneobunge la Suna Mashariki Kaunti ya Migori.

Shamba lake la ekari 2.01 humvunia tumbaku tani 1.6 kila mwaka.Mitende ana mkataba na Kampuni ya Kutengeneza Sigara na Bidhaa Nyingine za Tumbaku “British American Tobacco” (BAT).

BAT humpa mkopo wa pembejeo za kilimo na kununua tumbaku yake ambapo huondoa mkopo waliompa na kumtumia faida.

Mitende huuza kilo moja ya tumbaku kwa Sh150 na hupokea mkopo wa Sh40, 000 kutoka kwa BAT kila msimu.

“Niko tayari kuhamia ukuzaji wa maharagwe, hata shamba liko tayari, nasubiri nihakikishiwe soko lipo na nipigwe jeki kwani siko tayari kupoteza pesa ninayopata kutoka kwa tumbaku,” Mitende anasimulia.

Sehemu ya wakulima wa tumbaku wameripoti kuwa wamefikiria kuacha lakini wanapitia changamoto kutambua vitega uchumi mbadala vinavyofaa; hasa vile vinavyoweza kuwapa pesa mjarabu. Walioacha kukuza tumbaku wameingilia maharagwe, miembe, njugu, ndizi, mtama, mihindi, ufugaji kutaja tu baadhi.

Mkulima wa maharagwe Migori aondoa uchafu kwenye maharagwe aliyovuna. PICHA | LABAAN SHABAAN
  • Tags

You can share this post!

JIFUNZE BIASHARA: Ya kuzingatia wakati wa kutengeneza...

MITAMBO: Rain gun inatumia jua kuinyunyizia mimea yako maji

T L