• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
UJASIRIAMALI: Pikniki zake ni za kupigiwa mfano mijini

UJASIRIAMALI: Pikniki zake ni za kupigiwa mfano mijini

NA MARGARET MAINA

KWA njia nyingi, biashara yake ni tofauti na mtindo ambapo wanaoenda miadi au pikniki hubeba kila kitu wanachohitaji; kuanzia kwa viburudisho hadi vyombo, vikapu vya taka na blanketi ya kutandika chini katika mazingira ya nje ili kupata muda bora pamoja.

Kwa Njoki Mwangi, kumpangia rafikiye pikniki ndogo ili kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kulimpa wazo kwamba huu utakuwa mwanzo wa safari yake ya ujasiriamali.

Njoki, 25, ndiye mwanzilishi wa Picnics By Njoki, kampuni inayolenga kuwapa watu njia ya kipekee ya kusherehekea wapendwa wao kwa kupangiwa pikniki.

“Nilipokuwa nikimpangia rafiki yangu pikniki, nia yangu pekee ilikuwa kumpa siku ya kuzaliwa ya kukumbukwa. Hata hivyo, miezi kadhaa baadaye nikaona fursa ya kusambaza huduma zangu kwa umma,” asema Njoki.

Akiwa mhitimu wa shahada ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Daystar ambapo kwa sasa anasomea MBA yake ya fedha na usimamizi wa mikakati, Njoki hakufikiria kufanya biashara kama hiyo.

Yeye ni mkurugenzi wa fedha katika Kassmatt Supermarket.

“Ilikuwa baada ya utafiti mwingi ambapo nilijifunza na kukumbatia njia tofauti ambazo mtu anaweza kupeleleza na kupata maoni tofauti ya kuandaa hafla za nje kama vile pikniki,” akasema.

Njoki alishauriana na wazazi wake kwa kuwapangia pikniki Jumapili moja na pamoja na marafiki zake, waliunga Njoki mkono.

Kisha, alianza kununua fanicha, mito, shuka, na vifaa vyote vya pikniki, akitumia Sh120,000 katika shughuli hiyo. Kisha akaanzisha ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.

“Nilijiambia kuwa ikiwa biashara yangu haitafanikiwa, angalau nitakuwa na fanicha mpya na virembeshi vya nyumba yangu. Kwa mshangao, juhudi zangu zilipokelewa vyema,” anasema.

Njoki alizindua kampuni yake mnamo Septemba 2020, akilenga sherehe za siku za kuzaliwa.

“Baadaye nilipanua huduma zangu kwa hafla nzuri kama vile uchumba, sherehe za harusi na watoto pamoja na matukio ya kufichua jinsia.”

Baada ya muda mfupi, biashara yake ilikua na kwa sasa ana timu ya watu wawili, mmoja akiwa mchumba wake ambaye anakiri kuwa amemuunga mkono tangu kuanzishwa kwa biashara hiyo.

“Ninawapa wateja wangu orodha ya maeneo ambayo niliwahi kufanya kazi hapo awali, hasa bustani na bustani za kibinafsi jijini Nairobi na Kiambu. Mengi ya kumbi hizi ziko katika vitongoji tulivu na vina vyanzo vya maji ili kuleta mandhari mazuri.”

Pia kuna nyakati ambapo wateja hupendekeza kumbi tofauti, ambazo yeye hufanya kazi nazo.Vifurushi vyake vya mandhari ya Kiafrika vinakumbatia utamaduni wa Kiafrika kwa kutumia mapambo ya Kiafrika.

“Tuna matukio matatu ambayo natoza kima cha chini zaidi cha Sh3,500 kwa watu 4 ambapo na kwa watu 30, bei ni Sh35,000. Vifurushi vyetu huiga hali nzuri kutoka kwa mishumaa hadi divai hadi mapambo ya kifahari. Tuna uzoefu wa aina mbili, uzoefu wa kawaida na uzoefu wa juu – deluxe – ambao ni kati ya Sh4,000 hadi Sh45,000. Kifurushi cha uzoefu wa Boho-chic hutumia mtindo wa bohemian katika mapambo kutoka kwa Ottoman zilizosokotwa hadi vikapu vilivyofumwa. Tuna tajriba tatu, Mtindo wa Boho Teepee, Mtindo wa Boho Sunset na The Cinema Package, kuanzia Sh4,000 hadi Sh40,000.”

Kila kifurushi kinakuja na zulia la manyoya, usanidi wa mlo, na maonyesho ya maua.

“Ninakuwekea divai, vitafunio na vipande vya barafu huku nikitengeneza ujumbe kwenye ubao ili kuendana na hafla hiyo. Pia kuna muziki na mishumaa kwa hali kamili ya kuvutia. Kuongeza kuwa wanaoenda pikniki huleta chakula chao wenyewe.”

“Pia ninawapangia chakula kwa ombi kutoka kwa wachuuzi wanaowapenda,” anasema.

Wateja wake ni hasa kupitia kuambizana kutoka mtu mmoja hadi mwingine na kupitia mitandao ya kijamii.

Viti na meza ya kutumika katika pikniki. PICHA | MARGARET MAINA

Kupitia tajriba yake ya kipekee ya pikniki, Njoki analenga kuinua matukio madogo ya mkusanyiko wa mteja wake hadi matukio ya kukumbukwa.

Ili kufanikisha hili, yeye hufikia wachuuzi wa ndani kwa ajili ya vifaa kama vile fanicha na kuweka mipangilio iliyosalia na timu yake.

“Changamoto kubwa kwetu ni hali ya hewa isiyopendeza sana ambayo imewalazimu baadhi ya wateja wetu kukosa kwenda nje kabisa.”

Mjasiriamali huyu mchanga anatarajia kupanua biashara yake.Dhana yake imevutia hadi kampuni pia ingawa, anasema ana macho yake kwa wataalamu wa tabaka la kati na familia kama sehemu yake kuu ya soko.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Rain gun inatumia jua kuinyunyizia mimea yako maji

NJENJE: Mauzo ya miraa Somalia yazolea Kenya Sh220m kwa...

T L