• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
MUME KIGONGO: Mazoezi magumu kupindukia hupunguza hamu ya mapenzi

MUME KIGONGO: Mazoezi magumu kupindukia hupunguza hamu ya mapenzi

NA LEONARD ONYANGO

MAZOEZI ya viungo yana faida tele kwa afya yako. Mazoezi haya yanakuwezesha kupunguza uzani, kuboresha afya ya moyo, kupunguza msongo wa mawazo, kuimarisha kingamwili (immunity) na hata kuongeza hamu ya mapenzi.

Kwa mfano, tafiti zinaonyesha kuwa wanaume wanaofanya mazoezi ya viungo kwa dakika 30 kwa siku tano za wiki, wanaongeza hamu ya mapenzi na kuimarisha ubora wa mbegu za kiume.

Lakini wataalamu wanaonya kuwa kufanya mazoezi magumu kupindukia kama vile kubeba vyuma kwa muda mrefu kwa siku, ni hatari kwa afya yako.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa mazoezi ya viungo yawe ya wastani. WHO pia linapendekeza wanaume wazima kufanya mazoezi ya kadri kwa jumla ya saa tano kwa wiki au saa mbili na nusu kwa wiki kwa wanaofanya mazoezi magumu kiasi.

Tafiti zinaonyesha kuwa wanaume wanaofanya mazoezi magumu kupindukia kwa siku wako kata hatari ya kutatiza mfumo wa moyo, kusababisha kiharusi (stroke), kumaliza hamu ya mapenzi na kufifisha kingamwili.

Wataalamu wanasema kuwa mazoezi magumu kupindukia husababisha kingamwili kufifia kwa muda wa saa 72 hivyo kutia mwili katika hatari ya kushambuliwa na virusi na bakteria wanaosababisha maradhi.

Nao madaktari wanasema kuwa watu wanaofanya mazoezi magumu kupindukia wanajitia katika hatari kukumbwa na tatizo la uraibu wa mazoezi (exercise addiction).

Tatizo hilo husukuma waathiriwa kufanya mazoezi magumu kwa muda mrefu kila siku hivyo kuhatarisha afya zao. Dalili za tatizo hilo ni kuhisi uchovu unapokosa kufanya mazoezi na kuwa na hamu ya kufanya mazoezi hata kama unahisi maumivu.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Southern California, Amerika, ulibaini kuwa idadi kubwa ya wanaume walio na tatizo la uraibu wa mazoezi pia hujiingiza katika matumizi ya mihadarati.

You can share this post!

Ruto, Raila wakosa kipya cha kuahidi

JIJUE DADA: Chanzo cha vidutu kwenye tupu ya nyuma

T L