• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
NJENJE: Mauzo ya miraa Somalia yazolea Kenya Sh220m kwa siku 4

NJENJE: Mauzo ya miraa Somalia yazolea Kenya Sh220m kwa siku 4

NA WANDERI KAMAU

KENYA ilisafirisha miraa ya jumla ya Sh220 milioni siku nne za mwanzo tangu kurejelea uuzaji wa zao hilo nchini Somalia.

Wadadisi wanasema mapato hayo makubwa yanaashiria mchango wake mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.Kulingana na mkuu wa Idara ya Kusimamia Miraa, Pareto na mazao mengine ya kibiashara, Bw Felix Mutwiri, Kenya ilisafirisha jumla ya tani 81.4 za miraa tangu kufunguliwa upya kwa zao hilo.

Bw Mutwiri alisema kuwa wafanyabiashara 19 kati ya 22 waliokuwa wametuma maombi ya kupata kibali cha kuisafirisha, tayari wamepewa vibali hivyo. Aliongeza kuwa idadi hiyo inaendelea kuongezeka.

“Kufikia sasa, tumesafirisha jumla ya tani 81.4 za miraa. Tunatarajia kiwango hicho kuongezeka katika siku kadhaa zijazo, watu wengi wanapoendelea kupata kibali cha kuisafirisha,” akasema Bw Mutwiri.

Idara hiyo ilianza kutoa leseni za usafirishaji wa miraa wiki iliyopita, baada ya serikali ya Somalia kufungua upya soko lake.

Chini ya kanuni mpya, mtu yeyote ambaye atapatikana akisafirisha zao hilo bila leseni atakuwa hatarini kufungwa miaka mitatu gerezani au kupigwa faini ya Sh5 milioni.

Nchini Somalia, kilo moja ya zao hilo inauzwa kwa Sh2,734 bei ambayo ni ya chini ikilinganishwa na hapo awali, ambapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa Sh2,972 kabla ya soko hilo kufungwa.

Kenya inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka Ethiopia, ambayo imekuwa ikiiuzia Somalia zao hilo, baada ya Kenya kuzuiwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Miraa wa Nyambene (Nyamita), Bw Kimathi Munjuri, alisema kuwa kuna kiwango cha kutosha cha zao hilo nchini kukidhi mahitaji ya Somalia.

“Tuna kiwango cha kutosha cha zao hilo ambapo tunaweza kutosheleza hitaji la soko la Somalia bila tatizo lolote,” akasema Bw Munjuri.

Kwa miaka mitatu iliyopita, wafanyabiashara na wakulima wa miraa wamekuwa wakitegemea soko la hapa nchini, baada ya Somalia na Sudan kupiga marufuku uuzaji wake katika mataifa hayo mtawalia.

Hili ni kutokana na mzozo wa kidiplomasia ulioibuka kati ya Kenya na mataifa hayo.

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Pikniki zake ni za kupigiwa mfano mijini

Sonko ahemesha Omar kampeni za kusaka ugavana

T L