• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
PENZI LA KIJANJA: Ikiwa mnapendana, msisahau busu kwani hufanya miujiza

PENZI LA KIJANJA: Ikiwa mnapendana, msisahau busu kwani hufanya miujiza

NA BENSON MATHEKA

IWAPO unapanga kuoa au kuolewa katika maisha yako, usisahau kubusu mume au mke wako angalau mara mbili kwa siku.

Busu linafanya miujiza katika uhusiano japo kwa baadhi ya watu linaisha baada ya kulishana viapo vya ndoa.

Hata hivyo, waliobobea katika masuala ya ndoa wanasema kwamba wapenzi hawafai kuacha kupigana mabusu hata kama wamekuwa kwa ndoa kwa miaka mingi.

“Unapoamka, hata kama umekuwa katika uhusiano wa ndoa kwa muda mfupi au mrefu, busu mke wako, usimsalimie tu na kisha uende zako. Busu hilo huwa linatenda muujiza katika uhusiano ambao watu wengi wanakosa kwa kulipuuza,” asema mtafiti wa masuala ya mahusiano Jackie Adhiambo.

Busu halifai kutoka kwa mume pekee. Adhiambo anasema jioni, mume akifika nyumbani au wachumba wakikutana nyumbani, wanafaa kukaribishana kwa busu moto.

“Mumeo akifika nyumbani, usiketi chini. Amka na kumpokea katika mlango na kumkumbatia kisha umpige busu,” asema mtafiti huyu wa masuala ya mapenzi wa miaka mingi.

“Busu la mchumba hutuliza mtu na kumpunguzia shinikizo za kazi na shughuli za maisha. Busu linalotoka kwa mtu unayepatia moyo wako linakupatia nguvu za kumpenda zaidi. Ni hakikisho kwamba anaridhika kuwa nawe na anatambua mchango wako katika maisha yake,” aeleza Adhiambo.

Watalaamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba watu wengi huwa wanaacha kubusu wachumba wao katika awamu fulani ya kuishi pamoja jambo ambalo ni kupuuza kiungo muhimu cha kuongeza ladha uhusiano wao.

“Kwa watu kama hao, ni kama mapenzi huisha wakioa au kuoana. Kwa wanaojua muujiza wa busu na ladha linaloongeza kwa uhusiano wao, wanawapa wachumba wao angalau mara mbili kwa siku,” asema.

Busu moto huwa linalotoka ndani ya moyo, linatokana na msukumo wa hisia nzito za mapenzi na linachangia kuboresha tendo la ndoa. Adhiambo asema busu moto linapaswa kuandamana na kauli ya mapenzi kama ‘nakupenda’, ‘I couldn’t have married a better person…’ na kadhalika.

“Kila siku usisahau kubusu mtu wako na kumwambia ‘ninakupenda’ angalau mara mbili. Ukizoea hii, uhusiano wako hautakuchosha, utaimarika na utakuwa mtamu zaidi na bora,” asema mwanasaikolijia na mtaalamu wa masuala ya mapenzi Ruth Odili.

Kulingana na Ruth, hakuna mtu anayechoka kupata busu kutoka kwa mchumba wake likiambatishwa na kauli “ nakupenda”.

“Busu linaonyesha unajivunia na kutambua mchumba wako katika maisha yako. Muujiza linaoleta katika uhusiano wa kimapenzi ni mkubwa,” asema.

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Joho anavyomkweza Mboko kwa kususia hafla...

MALEZI KIDIJITALI: Mipaka idumu hata mtoto akiwa kwa...

T L