• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Polisi mchoraji ahimiza wenzake watumie talanta kuzima msongo wa mawazo

Polisi mchoraji ahimiza wenzake watumie talanta kuzima msongo wa mawazo

NA MAGDALENE WANJA

ELIJA Gakuya alikuwa tu amehitimu na cheti cha Kemia kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), alipoona tangazo kwenye gazeti kwamba kulikuwa na usajili wa maafisa wa polisi.

Bila kupoteza muda, alifika uwanjani siku ya siku na akabahatika kuwa mmoja wa wale waliosajiliwa wajiunge na kikosi cha polisi baada ya kufanyiwa majaribio.

“Nilipokuwa mdogo, ndoto yangu kubwa ilikuwa ni kuwa rubani wa ndege za kijeshi, ila sikufanya vyema katika somo la Fizikia. Pengine ndiyo maana nilipopata nafasi hii, nilihisi kwamba nimekaribia ndoto yangu,” anasema Gakuya.

Mnamo mwezi Mei 2017, alipewa kazi na akaanza kuhudumu katika kituo cha polisi cha Ngong.

Polisi mchoraji Elija Gakuya. PICHA | MAGDALENE WANJA

Alikuwa akiendelea na kazi na akaona fursa ya kutumia wakati wake wa kupumzika kuendeleza kitu alichopenda kukifaya tangu utotoni.

“Nilipokuwa mdogo nilipenda sana kuchora na walimu walivutiwa sana na michoro yangu na hivyo wakawa wananiwajibisha wakati wa kuchora michoro mbalimbali ikiwemo ramani wakati wa somo la Jiografia,” anasema Gakuya.

Kipaji kilikuwa na watu wengi wakaanza kuvutiwa sana na wakaanza kununua michoro yake.

“Kazi ninayoifanya mara nyingi huchosha sana. Kwa hivyo kila baada ya kazi, mimi huchora kama njia ya kupumzisha akili yangu,” anaongeza.

Mchoro wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ambao ni kazi ya sanaa ya Elija Gakuya. PICHA | MAGDALENE WANJA

Gakuya anasema kuwa kila anapopata nafasi, huwa anawazungumzia maafisa wenzake kuhusu umuhimu wa kutumia talanta kupumzisha akili na kujiongezea mapato.

“Kuna idadi kubwa ya maafisa wa polisi ambao hujitia kitanzi au kudhuru wenzao au familia, sababu kuu huwa msongo wa mawazo ama changamoto za kifedha. Kwa kutumia talanta, tunaweza kupunguza changamoto hii,” anadokeza Gakuya.

Mchoro wa mwigizaji wa Hollywood Lupita Nyong’o ambao ni kazi ya sanaa ya Elija Gakuya. PICHA | MAGDALENE WANJA

Kila mchoro una bei yake, ambapo afisa huyu anasema hutegemea ukubwa wake. Kwa ukubwa wa A4 bei ni Sh1,900 halafu Sh2,800 kwa A3, Sh4,500 kwa A2, na Sh7,000 kwa A1. Bei hii ikiwa ni pamoja na fremu.

Gakuya anatarajia kubadilisha maisha ya watu kupitia michoro yake.

Mchoro wa mwanamuziki Rick Ross ambao ni kazi ya sanaa ya Elija Gakuya. PICHA | MAGDALENE WANJA
Mojawapo ya kazi za sanaa za Elija Gakuya ambaye ni afisa wa polisi stadi wa kuchora. PICHA | MAGDALENE WANJA
Mchoro mwingine ambao ni kazi ya sanaa ya Elija Gakuya. PICHA | MAGDALENE WANJA
  • Tags

You can share this post!

Akothee ajitambulisha kama ‘singo matha’ licha ya...

Covid-19 ilivyogeuza ufugaji nguruwe kuwa kampuni

T L