• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Ruto pagumu kuwatosheleza ‘wageni wapya’

Ruto pagumu kuwatosheleza ‘wageni wapya’

NA WANDERI KAMAU

RAIS Mteule William Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu kutimiza ahadi alizotoa kwa washirika wake wa kisiasa, kutokana na idadi kubwa ya wanasiasa wanaoendelea kuhamia katika mrengo wa Kenya Kwanza.

Kwenye kampeni zake, Dkt Ruto aliahidi “kutowaacha nje” wanasiasa waliohangaishwa na serikali kwa “kuamua kuwa marafiki wake.”

“Tutabuni serikali kubwa itakayokuwa na nafasi kwa kila mmoja. Itakuwa nyumba kubwa ambayo itatoa nafasi kwa kila mmoja wetu,” akasema Dkt Ruto.

Hata hivyo, ongezeko la wanasiasa wanaoendelea kujiunga na mrengo huo limeibua wasiwasi miongoni mwa washirika wake, baadhi wakisisitiza kuwa hawatakubali watu waliojiunga nao katika dakika za mwisho mwisho “kugawiwa keki yao.”

Kufikia sasa, baadhi ya vigogo wa kisiasa ambao wamejiunga na kambi ya Dkt Ruto ni magavana wa zamani Kiraitu Murungi (Meru), James Ongwae (Kisii), mbunge David Ochieng (Ugenya), Seneta mpya wa Mandera Ali Roba kati ya wengine.

Katika kujiunga na Dkt Ruto, vigogo hao pia wamekuwa wakiandamana na jumbe kubwa za wanasiasa, baadhi yao wakiwa wagombeaji walioshindwa kwenye nyadhifa tofauti za kisiasa walizowania.

Malalamishi

Baadhi ya washirika wake ambao wamejitokeza kulalamikia idadi kubwa ya “wageni” wanaohamia kambi hiyo ni mbunge Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini), anayesisitiza kuwa kabla ya wanasiasa hao kuhamia Kenya Kwanza, Dkt Ruto tayari ana mikataba ya kisiasa na wale ambao wamekuwa pamoja naye.

“Tunawakaribisha wageni. Hata hivyo, lazima wafahamu kuwa wanaingia katika nyumba ambayo tayari ina wenyeji. Hivyo, lazima wafahamu kuwa hakuna mgao wowote wa mamlaka watakaopata,” akasema Bw Osoro, akionekana kumlenga Bw Ongwae.

Aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, pia ametoa kauli kama hiyo, akisema kuwa wale wanaotegemea kupata mgao wa serikali kwa kujiunga na Dkt Ruto “wamechelewa sana.”

Kulingana na wadadisi wa siasa, huenda mwelekeo huo ukaendelea kushuhudiwa katika siku chache zijazo, ikizingatiwa kuwa Dkt Ruto bado hajafanya teuzi muhimu kama uteuzi wa baraza la mawaziri, manaibu wao, wakuu wa mashirika tofauti ya serikali kati ya nyadhifa nyingine.

“Kibarua alicho nacho Dkt Ruto ni kuwarejeshea mkono washirika wake ambao wamekuwa naye kwa muda mrefu na kuwakaribisha wanasiasa wapya wanaohama kutoka mirengo kama Azimio na kujiunga naye. Ijapokuwa amesisitiza kuwa hatabuni handisheki na upinzani, bado atahitaji kupanua uungwaji wake mkono kisiasa. Ikumbukwe kuwa kama mwanasiasa, ataanza kubuni mikakati ya kuibuka mshindi katika muhula wa pili mara tu atakapoapishwa hapo Jumanne,” asema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kama njia ya “kuhakikisha uwazi” kwenye mikataba anayobuni na vigogo tofauti wa kisiasa, Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa “hatawahadaa washirika wake kama vile mrengo wa Azimio.”

“Tunatia saini mikataba yetu mchana wala si usiku kama washindani wetu. Vile vile, tunaiweka wazi. Hatumfungi wala kuwapa masharti washirika wanaojiunga nasi,” akasema Dkt Ruto, mara tu baada ya kutia saini mwafaka wa kisiasa na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko.

Hata hivyo, wadadisi wanaonya kuwa huenda Dkt Ruto akaanza kuwakasirisha baadhi ya washirika wake kutoka maeneo yaliyompigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

“Kwa maeneo kama Mlima Kenya, Dkt Ruto alikuwa ashabuni mikataba ya kisiasa nalo kuhusu vile atawagawia washirika wake nafasi muhimu kama uwaziri. Itamlazimu kutahadhari sana ili kutovuruga mikataba hiyo ili kuwapa nafasi wanasiasa wapya wanaojiunga naye,” asema mdadisi wa siasa Oscar Plato.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Itabidi watorokao Azimio ‘wajipange’

JUNGU KUU: Kibarua cha Raila na Uhuru kuokoa Azimio

T L