• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Itabidi watorokao Azimio ‘wajipange’

MIKIMBIO YA SIASA: Itabidi watorokao Azimio ‘wajipange’

NA CHARLES WASONGA

HUENDA kukatokea mvutano kati ya wanasiasa wanaogura muungano wa Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza na wandani wa zamani wa Rais Mteule William Ruto.

Hii ni baada ya baadhi ya wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza kuonyesha dalili za kutoridhishwa kwao na idadi kubwa ya wafuasi wa Azimio wanaojiunga na kambi yao siku chache kabla ya Dkt Ruto kuunda serikali mpya.

Wabunge, Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Oscar Sudi wanasema japo wanasiasa hao wanakaribishwa ndani ya Kenya Kwanza “wasitarajie kupewa viti vikubwa”.

“Mambo yamebadilika. Karibuni lakini mjue kwamba mtakaa nyuma yetu kwenye foleni. Mlituita watoto wakati huo lakini sasa msitarajie makubwa katika nyumba yetu,” akasema Bw Osoro.

Kwa upande wake, Bw Sudi anawataka viongozi wanaogura Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza kufahamu kwamba “tayari tulikuwa tumejipanga na wasije kupangua mipango yetu.”

“Tumefurahi kwamba wabunge wenzetu wa upande wa Azimio walifanya jambo la busara kwa kuungana nasi na tukaweza kushinda viti vya uspika na unaibu spika katika bunge la kitaifa na seneti. Lakini wajue kwamba kama Kenya Kwanza tulikuwa tumejipanga zamani,” Bw Sudi alisema siku moja baada ya shughuli hiyo ya uchaguzi kukamilika.

Katika Bunge la Kitaifa aliyekuwa Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula alishinda kiti cha uspika huku Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu Gladys Boss Shollei akichaguliwa kama Naibu Spika.

Katika Seneti aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi alishinda wadhifa wa uspika huku Seneta wa Meru Kathuri Murungi akitunukiwa kiti cha Naibu Spika.

Mrengo wa Kenya Kwanza ulipata ushindi wa urahisi kufuatia hatua ya wabunge na maseneta wa vyama tanzu katika Azimio kuhamia mrengo huo unaoongozwa na Dkt Ruto.

Kenya Kwanza ilipigwa jeki na wabunge na maseneta kutok vyama kama vile; United Democratic Movement (UDM), KANU, Pamoja African Alliance (PAA), Movement for Development and Growth (MDG), ambavyo ni vyama tanzu katika Azimio.

Kisheria Azimio ina wabunge 174 huku Kenya Kwanza ikiwa na wabunge 164.

Hii ina maana kuwa wabunge wa Azimio waliojiunga na Kenya Kwanza watachukuliwa kama “waasi” na hivyo watanyimwa nafasi katika kamati za bunge.

Ndiposa Bw Sudi anawaonya kwamba wasitajie kutunukiwa nafasi zilizotengewa wabunge wa Kenya Kwanza.

Aidha, Mbw Sudi na Osoro wamewaonya magavana wa zamani waliokuwa mrengo wa Azimio na sasa wameamua kujiunga na Kenya Kwanza, kwamba wasitarajie “makubwa”.

“Hao ambao wanajiunga nasi sasa wasifikirie kuwa watapewa viti vikubwa na watu wetu wanaachwa nje,” anasema Bw Osoro, akionekana kurejelea magavana wa zamani Kiraitu Murungi (Meru) na James Ongwae (Kisii).

Bw Osoro alitoa kauli hiyo saa chache baada ya aliyekuwa Gavana wa Kisii James Ongwae na wanasiasa wengine kutoka eneo la Gusii waliopoteza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kugura Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza.

Ijumaa asubuhi, viongozi hao kutoka kaunti za Kisii na Nyamira walikutana na Dkt Ruto katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi katika kile kilichoonekana kama mwanzo wa ushirikiano kati yao na serikali mpya.

Wengine walioandamana na Bw Ongwae ni; aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Chris Obure, aliyekuwa Mwakilishi wa Kike Kisii Janet Ong’era, wabunge wa zamani Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache Kaskazini), Richard Tong’i (Nyaribari Chache), Ben Momanyi (Borabu), Manson Nyamweya (Mugirango Kusini) na Zadock Ogutu (Bomachoge Borabu).

Bw Ongwae na Bi Ong’era wamekuwa wandani sugu wa aliyekuwa mgombea urais wa Azimio Raila Odinga kwa miaka mingi.

You can share this post!

WALIOBOBEA: Ndwiga, waziri mtulivu aliyechapa kazi vyema

Ruto pagumu kuwatosheleza ‘wageni wapya’

T L