• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Sabina Chege alia waheshimiwa bungeni kumuibia simu aina ya iphone 14

Sabina Chege alia waheshimiwa bungeni kumuibia simu aina ya iphone 14

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE maalum Sabina Chege amedai kuwa simu yake yenye thamani kubwa, iliibwa bungeni.

Bi Chege, alisema alinyang’anywa simu aina ya iphone 14 mnamo Juni 8, 2023 kufuatia vurugu zilizozuka katika bunge la kitaifa.

Akizungumza eneo la Meru, mbunge mwakilishi huyo wa wanawake zamani Murang’a, alimrai Naibu Rais Rigathi Gachagua kuingilia kati kumsaidia kupata simu hiyo.

“Mbali na kunivamia na kunipiga, walinipora simu aina ya iphone 14. Ninakuomba Mheshimiwa Naibu Rais Rigathi Gachagua unisaidie nirejeshewe simu yangu,” Bi Sabina alimwambia naibu rais katika kongamano la kahawa lililohudhuriwa na Bw Gachagua kujadili mikakati kuboresha kilimo na soko la zao hilo nchini.

Sabina ambaye ni naibu kiranja wa wachache bungeni, aliteuliwa kama mbunge maalum kupitia chama cha Jubilee, na alilaumu wabunge wa upinzani Bi Millie Odhiambo (Suba Kaskazini) na Rosa Buyu wa Kisumu Magharibi, kupotea kwa simu yake.

Siku ya tukio, wabunge wa muungano wa upinzani, Azimio la Umoja na wa Kenya Kwanza walizozana, Azimio ikimtaka spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula kumvua Bi Sabina Chege wadhifa wa naibu kiranja wa wachache.

Sabina kwa sasa anaunga mkono serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, licha ya kuteuliwa kuingia bungeni kupitia chama cha Jubilee ambacho ni miongoni mwa vyama tanzu vinavyounda Azimio.

Katika uchaguzi mkuu 2022, Sabina aliunga mkono Bw Odinga kuingia Ikulu.

Upinzani unamtaka mbunge huyo kung’atuka, kwa kile wanalalamikia kama kukosa nidhamu chamani na kutokuwa mwaminifu kwa Jubilee.

“Ninaomba walioniibia simu wairejeshe tu,” Sabina aliwarai.

Kwa upande wake Bw Wetangula, alikataa kubandua mbunge huyo akihoji mikono yake imefungwa na amri ya korti inayolinda Bi Sabina.

Kufuatia zogo la waheshimiwa siku ya drama bungeni, spika Wetangula aliwapa marufuku ya muda wa majuma mawili na wengine siku tano, wabunge saba wa Azimio, Sabina akiwemo.

Wengine walioathirika na amri hiyo ni Bi Millie Odhiambo, Rosa Buyu, TJ Kajwanga wa Ruaraka, Catherine Omanyo (Busia), Joyce Kamene (Machakos) na Amina Mnyazi wa Malindi.

Bi Rosa, hata hivyo, alidai kwamba marufuku hiyo ni njama ya serikali ya Kenya Kwanza kupitisha Mswada tata wa Fedha 2023.

Upinzani ukioongozwa na kinara wa Azimio, Raila Odinga umeapa kutumia mbinu zote kuangusha mswada huo unaopendekeza nyongeza ya VAT, ikiwemo ya mafuta na asilimia 3 ya mshahara wa kila mfanyakazi kukatwa kwa minajili ya mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

  • Tags

You can share this post!

Msanii Mammito alia kwa kuzuiwa kuingia Ikulu Nairobi

Waziri Kindiki aonya kuhusu maandamano kupinga Mswada tata...

T L