• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
Tabia na hali zinazohusishwa na ugonjwa wa mishipa ya moyo na namna unavyoweza kuzirekebisha

Tabia na hali zinazohusishwa na ugonjwa wa mishipa ya moyo na namna unavyoweza kuzirekebisha

NA MARGARET MAINA

[email protected]

Kuwa na uzani kupindukia

KUWA na uzani au uzito wa ziada kunaweza kusababisha kuongezeka kwa lehemu mbaya, shinikizo la damu na kupunguza kiwango cha lehemu inayofaa na hivyo kuongeza ugonjwa wa moyo na mishipa.

Kwa bahati mbaya, kupunguza uzito ni vigumu zaidi tunapozeeka.

Jinsi ya kurekebisha:

Kuuchukua udhibiti wa sababu za hatari za ugonjwa wa moyo kunaweza kusaidia kuwezesha kupunguza uzito. Hata hivyo, unapaswa pia kuzungumza na mtaalamu wa afya ili kuwa na mpango wa kupoteza uzito ili kuafikia malengo ya kibinafsi.

Kuangalia uzito mara kwa mara kunaweza kukusaidia kudhibiti uzito. Na ingawa mabadiliko ya kila siku yanatokea, kuweka kumbukumbu kwa uzito kunaweza kusaidia kutambua mwelekeo wowote wa kupata uzito katika kipindi cha muda.

Mazoea ya kula vyakula vilivyosindikwa

Ingawa chipsi ni tamu na mtu anaweza kuzila kila mara bila ‘kuchoka’, lishe ambayo hujazwa na vyakula vilivyochakatwa sana huwa na mafuta mengi, ambayo yote yamehusishwa na ugonjwa wa moyo.

Zaidi ya hayo, chumvi nyingi katika lishe inaweza kuongeza viwango vya shinikizo la damu. Kujumuisha lishe yenye kalori nyingi pia huongeza hatari ya mtu kupata uzito na unene kupita kiasi, na hivyo kuongeza hatari ya ugonjwa wa moyo na mishipa.

Jinsi ya kurekebisha:

Epuka chakula kilichochakatwa sana na badala yake uzingatie lishe yenye afya na salama kwa moyo na mishipa. Unaweza ukala nafaka, matunda na mboga mboga, maharagwe na kunde, na karanga. Samaki pia ni tegemeo kuu ikiwa unataka lishe muhimu kwa afya ya moyo. Vile vile unaweza ukala kuku konda kiasi cha wastani, bata mzinga, na nyama ya ng’ombe.

Watu binafsi wanahimizwa zaidi kupunguza vyakula vilivyochakatwa sana ambavyo huwa vinajazwa na sukari, chumvi, na viambajengo vingine.

Kuishi maisha ya kuketi kwa muda mrefu

Kuishi maisha ya kuketi chini kumehusishwa na kunenepa kupita kiasi, shinikizo la damu, lehemu ya juu, na magonjwa mengine sugu.

Ingawa hivyo, mazoezi ya kawaida ya mwili yanaweza kupunguza hatari yako ya ugonjwa wa moyo kwa kuboresha mtiririko wa damu, pamoja na kudhibiti uzito ili kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo, kiharusi, na shinikizo la damu.

Jinsi ya kurekebisha:

Shiriki katika angalau dakika 30 za mazoezi kila siku.

Jishughulishe na mpango wa mazoezi pamoja na kushauriana na mtaalamu atakayekupa vidokezo muhimu.

Kuvuta sigara

Uvutaji sigara ni uraibu na tabia inayohusishwa na ugonjwa wa moyo na mishipa. Hii ni kwa sababu moshi huingilia mtiririko wa damu na oksijeni kwa ubongo. Uvutaji sigara unaweza pia kusababisha mkusanyiko wa mafuta kwenye mishipa, kuongeza shinikizo la damu, kupunguza uvumilivu mtu anapofanya mazoezi, na pia kupunguza uwezo wa damu kuganda.

Kukabiliwa na moshi wa sigara kutoka kwa watu wengine kunaweza pia kuongeza hatari ya ugonjwa wa moyo hata kwa wasiovuta.

Jinsi ya kurekebisha:

Hakuna njia nyingine ya kuishughulikia: Ikiwa unavuta sigara, wakati mzuri wa kuacha ni sasa hivi; tena mara moja. Ukichukua hatua ya kuacha sigara utakuwa umefaidika na afya ya mwili wako mwenyewe, lakini pia utakuwa umezingatia afya ya wengine kwa kupunguza moshi wa sigara.

  • Tags

You can share this post!

Vyakula bora vya kusaidia kuimarisha umeng’enyaji wa...

Manufaa ya mafuta ya mbegu nyeusi ambazo kwa jina la...

T L