• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
‘Tunataka stima madhubuti 2024’

‘Tunataka stima madhubuti 2024’

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI, viongozi na wanaharakati wa kijamii kaunti ya Lamu wameililia serikali kupitia Kenya Power kuhakikisha miundomsingi muhimu inakarabatiwa na kusitisha kupotea kila mara kwa stima eneo hilo.

Tangu Septemba 2023, Kaunti ya Lamu imekumbwa na changamoto ya kupoteapotea kwa stima karibu kila siku, hali ambayo imewaacha wafanyabiashara wakikadiria hasara ya bidhaa zao kuharibika, hasa zile zinazohifadhiwa majokofuni.

Kwenye kikao na wanahabari kisiwani Lamu, wakazi na wanaharakati wakiongozwa na seneta maalum, ambaye pia ni mzawa wa Lamu, Bi Shakila Abdalla, waliipa serikali na Kenya Power makataa ya siku 14 kurekebisha hitilafu hiyo.

Bi Shakila alitaja kupotea kiholela kwa stima kila mara kuwa mbinu ya serikali na Kenya Power kuendelea kuibagua, kuitenga na kuitelekeza Kaunti ya Lamu kihuduma.

Bi Shakila alishinikiza kuhamishwa kwa wasimamizi wa kampuni ya Kenya Power wanaohudumia Lamu kwa misingi ya utepetevu.

“Sisi tumechoka na hii hulka ya Kenya Power kupoteza stima ovyoovyo. Sekta karibu zote hapa Lamu, iwe ni biashara, utalii na hata uvuvi, vyote vimeathiriwa na stima kupoteapotea. Licha ya kulalamika kila mara ukarabati wa kudumu ufanywe, Kenya Power imetudharau na kuachwa tukihangaika. Tumetoa makataa ya wiki mbili kwamba warekebishe hali hii kufikia January 7,2024 la sivyo tuandamane kulazimisha wakuu wa Kenya Power wa hapa Lamu waondolewe. Tunataka stima madhubuti mwaka 2024,” akasema Bi Shakila.

Bi Raya Famau ambaye ni Mkurugenzi wa Muungano wa Wanawake wa Lamu Women Alliance, alisema ukosefu wa stima umeathiri hata sekta ya afya, hasa kwa akina mama wanaojifungua hospitalini.

Bi Famau alisema wanawake wengi wanaojifungua, hasa kupitia upasuaji hospitalini, wamejipata pabaya punde operesheni ya upasuaji inapoendelea na kisha stima kupotea.

Isitoshe, majenereta na mashini nyingine zinazotumiwa kuhudumia wagonjwa hospitalini zimeharibika kabisa, hasa tangu stima ilipoanza kukatikakatika.

“Tayari tuna ripoti za vifaa vya hospitalini kama vile mashini ya CT Scan, majenereta, zile za kusafisha figo,ambazo zote zimeharibiwa na hii stima ya kupoteapotea. Twataka mabadiliko. Watuletee umeme dhabiti 2024 ama wahusika wahame hapa Lamu tuletewe wengine wa kutuzingatia vilio vyetu. Tumechoka kulalamika ilhali watu wakitutelekeza,” akasema Bi Famau.

Abdalla Sharif, mmoja wa wafanyabiashara wa maduka ya jumla kisiwani Lamu, alisema ipo haja ya kukatika kiholela kwa stima kurekebishwa na Kenya Power pamoja na serikali kuzingatia kuwafidia wote waliopoteza bidhaa zao kutokana na hitilafu ya kila mara ya stima kote Lamu.

“Yaani siku haiishi hapa Lamu bila ya stima kupotea, iwe ni kwa muda wa saa tatu, sita, saba, tisa au hata siku nzima. Hili limechangia hasara kubwa kwetu kwani bidhaa za kwenye masanduku ya barafu au friji huishia kuoza. Vyombo vya kielektroniki, zikiwemo redio, televisheni, na friji zimekuwa zikichomeka kila mara hitilafu ya umeme inapotokea. Warekebishe hali hiyo na pia tufidiwe,” akasema Bw Sharif.

Msikiti Rodhwa ulioko katika kisiwa cha Lamu. Kupotea kiholela kwa umeme pia kumeathiri ibada misikitini, hasa nyakati za kuswali usiku. PICHA | KALUME KAZUNGU

Katika mahojiano ya awali na Taifa Leo, Meneja wa Mauzo wa Kenya Power katika Kaunti ya Lamu, Bw Bernard Kataka, alisema changamoto ya kila mara ya kupotea kwa stima katika Kaunti ya Lamu itaendelea muda mrefu, hasa kufuatia tukio ambapo magaidi wa Al-Shabaab walipiga na kuharibu mnara mkuu wa laini ya stima ya nguvu za juu za 220KV.

Shambulio na uharibifu huo uliotekelezwa asubuhi ya Septemba 24, 2023.

“Tukio la kigaidi la Septemba ndilo lilichangia kuharibiwa kwa mnara wa 220KV, hivyo kulazimu eneo hili la Lamu kuhudumiwa na stima ya kiwango cha 33KV ambacho ni kiwango kidogo. Kutokana na ughali wa mnara huo wa 220KV, itatulazimu kuvumilia matatizo lakini timu yetu itafanya kila jitihada kuona kwamba angalau stima inasambazwa Lamu hadi pale ukarabati wa kudumu utakapofanywa,” akasema Bw Kataka.

  • Tags

You can share this post!

Sabina Chege: Kwa Pasta Ng’ang’a ndipo

Ninaenda ‘break’ mashabiki mnisubiri – Akothee

T L