• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
UFUGAJI: Nguruwe wampatia maisha mapya baa iliposambaratika

UFUGAJI: Nguruwe wampatia maisha mapya baa iliposambaratika

NA LABAAN SHABAAN

ANNASTACIA Gakuyu aliacha biashara ya baa mwaka wa 2020 baada ya kuathiriwa na mlipuko wa corona na kuingilia ufugaji wa nguruwe.

Alipigwa na msongo wa mawazo kwa kwa kuwa ilikuwa biashara aliyotegemea kwa miaka mingi. Hata hivyo, sasa anahisi ufugaji na kilimo utamsaidia kimaisha kwani anahisi mbele kuna matumaini.

Alipata vidokezo vya ufugaji wa nguruwe kwenye mtandao wa YouTube na kushauriwa na wakulima wengine kisha akanunua nguruwe wawili waliokuwa karibu kuzaa kwa Sh60,000.

Akilimali inapoingia katika shamba la Grace Farm wadi ya Kahawa West eneobunge la Roysambu, Kaunti ya Nairobi, tunamkuta Gakuyu na wafanyakazi wake watatu wakilisha nguruwe.

“Tumemaliza kusafisha mabanda ya nguruwe hawa sasa hivi na ni wakati wa kuwalisha. Biashara hii ilianza kwa neema ndiyo maana naiita Grace Farm. Huu ni mwanzo, mwaka kesho nitakuwa nafuga maelfu ya nguruwe,” Gakuyu anasema.

Mama huyu wa watoto wanne anaeleza kuanza biashara hii kulimgharimu angalau Sh100,000 na miaka mitatu baadaye anaendelea kupokea hundi ya Sh400,000 kutoka kwa kampuni ya Farmers Choice kila baada ya miezi miwili.

Gakuyu anafuga nguruwe 80 kwenye shamba la robo ekari katikati ya makazi ya watu. Anasema kelele za nguruwe na pengine harufu ya shambani itawasumbua majirani kwa hivyo anapanga kuhama mwaka 2023.

“Nina uhusiano mzuri na Benki ya Equity ambapo napanga kupata mkopo kutumia hati ya ardhi na kuendesha ufugaji huu katika shamba la ekari mbili na zaidi. Natazamia kuwa na shamba la nguruwe la kisasa zaidi,” Gakuyu anaarifu.

Ili kuhakikisha yuko sokoni kila baada ya mwezi mmoja, Gakuyu huhakikisha ana nguruwe katika hatua tofauti za ukuaji.Kuna wale wachanga wanaonyonya, walioachishwa kunyonya na wale waliotayari kufika sokoni wenye uzani wa takribani kilo 70.

“Hunigharimu wastani ya Sh10, 000 kulisha nguruwe na kutunza kutoka udogoni hadi afike umri wa kuwa tayari kuuzwa baada ya miezi sita. Mimi huuza nguruwe kwa Sh21,000,” Gakuyu anaeleza.

Kulingana na utafiti wake, aliona wakulima wengi wamechagua nguruwe aina ya Landrace na Large White kuzidisha mapato. Gakuyu anasema yeye hufuga aina hii ya nguruwe kwa sababu wana ubora katika kuzaa na utunzaji wa watoto.

Mfugaji nguruwe Annastacia Gakuyu katika banda la nguruwe Wadi ya Kahawa West, Nairobi. PICHA | LABAAN SHABAAN

Aghalabu mkulima huyu hununua lishe ya nguruwe kutoka kwa kampuni ambayo hununua nguruwe wake wakikomaa. Kadhalika Gakuyu hukuza mboga aina ya spinach na sukuma wiki katika shamba lake ili kulisha nguruwe. Kinyesi na uchafu shambani hutumiwa kuwa mbolea.

Gakuyu anaambia Akilimali kuwa anahitaji kuwa makini kudumisha usafi kuendesha zaraa hii. Langoni, utakatishaji unahitajika kuzuia msambao wa magonjwa.

Pia anahofu kuhusu magonjwa kwani endapo yatalipuka hasa maradhi ya homa ya nguruwe, yataleta hasara kubwa. Siri yake kubwa anasema ni kuwa na uhusiano mzuri na madaktari wa mifugo na kuchukuwa tahadhari.

Japo kufikia sasa Gakuyu hajapitia changamoto vile, anaona kuna haja ya kupanuliwa kwa soko la nguruwe kwa sababu anahisi wafugaji wanaongezeka kila kuchao.

Gakuyu atakapopanua shamba lake, ana nia ya kuanza bucha ya nyama ya nguruwe.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Wakenya wasitarajie makuu kutokana na ahadi...

UJASIRIAMALI: Huduma za arafa zimemjengea jina

T L