• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
UJASIRIAMALI: Msanifu stadi, kazi ameweka blockcheni

UJASIRIAMALI: Msanifu stadi, kazi ameweka blockcheni

NA MARGARET MAINA

WAKATI hafanyi kazi na Naivaa, chapa ya mitindo aliyoianzisha alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Manchester, Joel Meshak, 25, anatengeneza sanaa ya kidijitali ambayo huiuza kwenye mtandao.

Miundo yake ya ubunifu inapatikana kama Non-Fungible Tokens (NFTs) na huhifadhiwa kwenye blockchain, leja ya dijitali ya aina ambayo haiwezi kubadilishwa.

“Nilianza kubuni nguo mwaka wa 2015 kabla ya kuamua kuanzisha chapa ya ‘Naivaa’ mwaka wa 2017. Kilichoanza kama hitaji hili la asili la kubuni nguo zangu kikageuka kuwa njia kwangu kueleza bayana ujumbe na kuleta mabadiliko ya kijamii kupitia biashara niliyoanzisha ya mitindo,” anasema Joel.

Katika miaka miwili ya kwanza, Meshak alilenga kujenga chapa yake kwa kutengeneza makusanyo mengi tofauti.

“Kwa mkusanyiko wa kwanza nilipata wawekezaji wadogo ambao waliwekeza Sh150,000. Hii ilishughulikia kundi la kwanza la hoodies 60 na vitambaa vya kitenge, ambavyo nilivitumia kubinafsisha vipande. Tangu wakati huo nimeweza kufadhili makusanyo kutokana na faida iliyopatikana kwa biashara hiyo.”

Bei za bidhaa ya Naivaa ni kati ya Sh1,000 na Sh5,000, cheni na kofia za baseball ni Sh1,000,hoodies ni kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000 kulingana na nyenzo, miundo na ubinafsishaji.

Hadi sasa, wameuza bidhaa zaidi ya 500.

Kazi mojawapo ya sanaa ya kidijitali anayouza Joel Meshak mtandaoni. PICHA | MARGARET MAINA

Anasema kwamba wanalenga soko lao kupitia Instagram kwa kutumia video za dhana ya ubunifu kwa kampeni za uuzaji.

“Nilielekeza video na kubuni mchoro wa sanaa. Polepole nilivutia wateja kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii na nikaanza kufanya mauzo kwa sababu watu waliunganishwa na ujumbe ambao tunaeneza kupitia vipande vyetu.”

Kwa sasa, Meshak hajawaajiri wafanyakazi wowote kwani anapohitaji huduma fulani, yeye huajiri au kusaini mikataba ya muda mfupi.

“Tumeweza kutoa ufahamu kuhusu masuala fulani ya kijamii na kuanzisha lugha mpya ya kubuni ambayo inawakilisha Nairobi kwa njia chanya ili kutoa mwanga katika tasnia ya ubunifu,” asema akiongeza kuwa kupitia kampeni zao, Naivaa imewapa fursa wanamitindo, wapiga picha na wasanii wengine sio tu kupata mapato kutokana na ufundi wao bali pia kupata uzoefu na kujifunza kutoka kwao.

Anadai kuwa, kuna hatua nyingi za kuunda na hatimaye kuuza vipande vya sanaa vya dijiti, ambavyo anasema vyake, vimechochewa na maisha yake ya kibinafsi, ya kibiashara na kijamii, vinaundwa kupitia upigaji picha na videografia na vinalenga kusherehekea utamaduni wa watu weusi.

Ingawa imekuwepo kwa muda, NFTs ilivutia Wakenya mnamo 2021 habari zilipoibuka kwamba mwanariadha aliyevunja rekodi Eliud Kipchoge alikuwa ameuza NFTs zake kwa Sh4 milioni.

“Sikuwa nimesikia kuhusu NFTs kabla ya 2021. Motisha kubwa ilikuwa kuona watu wengine wakipata pesa kupitia sanaa ya kidijitali. Lakini baada ya muda niligundua kuwa kuna mengi zaidi: unapata miunganisho, unakutana na wasanii wapya na kwa ujumla unajenga jumuiya halisi mtandaoni,” anasema.

Meshak anasema kuwa NFTs huwapa wasanii fursa mbalimbali kupata riziki kimataifa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Kazi ilikosekana, akajipa ya ukulima na wala hajuti

CDF: Wabunge watisha kuangusha bajeti ya ziada

T L