• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
UJASIRIAMALI: Ufugaji sungura wenye tija

UJASIRIAMALI: Ufugaji sungura wenye tija

NA MARGARET MAINA

[email protected]

UFUGAJI wa sungura nchini Kenya unaendelea kuimarika kila siku.

Siku hizi sungura hufugwa si tu kama wanyama wa kufurahia kuwaona nyumbani au kwa ajili ya nyama pekee, lakini pia kwa sababu wana umuhimu mwingine.

Bila shaka unafahamu kwamba sungura ni watoaji wa mbolea ya bei nafuu na ya gharama nafuu. Mkojo wao unaweza ukachukuliwa kama ni taka, lakini kwa James Kibuku,50, anapata ajira kutoka kwa sungura wake.

Kibuku hupata faida ya kila mwezi ya zaidi ya Sh100,000 kutokana na mkojo wa sungura. Vile vile hujiongezea faida kwa kuuza nyama ya sungura na kinyesi chake kama mbolea.

Yeye huuza sungura wake wa umri wa miezi mitatu kwa Sh2,500 nao sungura wa kike waliokomaa akiwauza kwa Sh5,000 na sungura wa kiume Sh4,500 kila mmoja.

Nyama mbichi ya sungura. PICHA | MARGARET MAINA

Nyama ya sungura yeye huiuza kwa Sh1,000 kwa kilo lakini ikiwa ni nyama choma yeye huiuza Sh1,500 kwa kilo.

Alianza biashara yake na sungura 10 pekee mwaka wa 2017, ambapo kila mmoja alimgharimu Sh350 lakini leo hii anajivunia kumiliki sungura 370.

Ndoto yake hata hivyo ni kumiliki sungura 1000 ifikapo mwisho wa mwaka huu 2023.

“Ufugaji wa sungura sio kazi ngumu kama wa ng’ombe na kuku. Ni rahisi kuwalisha sungura na mara nyingi huhitaji kuchukua tahadhari ya hali ya juu,” asema.

Tofauti na mifugo mingine, sungura sio wanyama wanaohitaji rasilimali nyingi na nyama yao inachukuliwa kuwa konda (mafuta kidogo) na yenye afya sana.

Shamba la Kibuku linapatikana katika eneo la Engashura, Kaunti ya Nakuru.

“Nilianza na sungura kumi kwa nia ya mbolea katika shamba langu huko Laikipia. Lakini kadri walivyoongezeka, niliona umuhimu wa kuwashirikisha wakulima wengine wajue umuhimu wa mkojo unaotumika kama mbolea ya mimea na dawa ya kuua wadudu,” anasema.

Anauza lita moja ya mkojo wa sungura kwa Sh100. Wateja wake huenea hadi nje ya nchi. Anasafirisha mkojo huo hadi nchini Botswana ambako pia kuna wateja wake.

Sungura mmoja humpa takriban mililita 100 za mkojo kila siku. Kwa shamba la Bw Kibuku ambalo lina sungura wapatao 370, hii inamaanisha takriban lita 37 za mkojo wa sungura kila siku.

Sungura wakiwa kizimbani. PICHA | MARGARET MAINA

Kwake usafi ni muhimu. Kizimba chake cha sungura kina matundu ya waya chini na bati zilizounganishwa kwenye mfereji unaoupeleka mkojo kwenye ndoo ya kukusanya.

“Banda la sungura hujengwa kwa njia ambayo mkojo hupenya kupitia wavu wa waya, kwenye bati hadi kwenye mfereji ambao huumwaga ndani ya ndoo ya kukusanya. Inachukua sungura watatu hadi wanne kukusanya lita moja ya mkojo kwa siku kupitia banda lililoundwa mahususi ili kuwezesha ukusanyaji,” anasema.

Kisha anachuja mkojo kwenye chombo kikubwa zaidi ambacho huwekwa tayari kwa kuuzwa.

“Ufugaji wa sungura wenye mafanikio unategemea miundo sahihi katika utengenezaji wa vizimba. Lishe sahihi lazima izingatiwe kuanzia wakati sungura wakiwa wadogo hadi kipindi cha ukomavu,” asema.

Bw Kibuku anawahimiza vijana na makundi mengine ya wanajamii kukumbatia ufugaji wa sungura na kuwataka wajisajili kwa Sh1,000 kila mmoja ambapo atawafunza kila Jumamosi mbinu za utunzaji sungura, ujenzi wa banda na kuwapa ujuzi wa kuzalisha mapato.

Ananuia kuangazia kikamilifu ufugaji wa sungura wa kiwango kikubwa ifikapo mwisho wa mwaka na kupanua vizimba vyake ili kuchukua sungura wengi zaidi.

Nyama ya sungura ina kiasi kikubwa cha protini zinazoweza kumeng’enywa na lehemu na mafuta ya chini zaidi ya aina zote za nyama. Sungura pia ni rahisi kufuga na huhitaji mtaji mdogo.

  • Tags

You can share this post!

Je, unapaswa kuosha uso wako kwa maji baridi?

KICD kuchapisha vitabu zaidi ya milioni 15 vya Gredi ya 7

T L