• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
WALIOBOBEA: Sambili: Mwanamke wa kwanza Mtugen kuwa mbunge, waziri

WALIOBOBEA: Sambili: Mwanamke wa kwanza Mtugen kuwa mbunge, waziri

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

MNAMO Desemba 29, 2007 gazeti ya Daily Nation lilikuwa na habari yenye kichwa ‘Uchaguzi wapeleka wanawake zaidi katika bunge la Kumi’.

Habari hizo ziliangazia eneo la Rift Valley ambako wanawake sita walikuwa wamewashinda wanasiasa wa miaka mingi katika uchaguzi mkuu uliofanyika siku mbili zilizokuwa zimetangulia.

Miongoni mwa washindi alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Egerton Hellen Jepkemoi Sambili ambaye alimshinda Joseph Korir kama Mbunge wa Eneobunge la Mogotio kaunti ya Baringo.

Aliungana na wanawake wengine 15 waliochaguliwa Bungeni katika uchaguzi mkuu wa Desemba 2007, baada ya kuwashinda wagombeaji wengine watano wanaume kwa tikiti ya chama cha kisiasa ambacho hakikuwa kikifahamika sana cha United Democratic Movement (UDM).

Ni muhimu kufahamu kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 1997, eneobunge la Mogotio lilikuwa limewakilishwa na chama cha Kenya African National Union (KANU) — na hivyo basi lilichukuliwa kuwa ngome ya KANU.

Alihimili ushindani, ghasia na hongo na desturi viongozi walipaswa kuwa wanaume na kuwa mwanamke wa kwanza kutoka jamii ya Tugen (mojawapo ya jamii ndogo za Kalenjin) kuchaguliwa kuwa mbunge.

Sambili alikuwa mbunge wa pekee wa chama cha UDM katika Bunge la Kumi (2008–2013). Ufanisi huu, ulivyokuwa wakati huo, ulikuwa mwanzo wa safari ya kisiasa yenye mawimbi ya Sambili na katika serikali.

Lakini muhimu zaidi, ilidhihirisha uvumilivu wa Rais Mwai Kibaki na uwezo wake wa kuepuka ubinafsi katika Serikali ya Muungano wa Kitaifa.

Kabla ya kujiunga na siasa, Sambili, aliyezaliwa 1959, alikuwa msomi katika Chuo Kikuu cha Egerton, kimojawapo cha Vyuo Vikuu vya Umma.

Alikuwa amefunza katika shule za sekondari ikiwemo Moi High School, Kabarak. Mwaka wa 2008, aliteuliwa waziri wa Michezo na Masuala ya Vijana katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano wa Kitaifa, na kujiunga na wanawake wengine 12 walioteuliwa kuwa mawaziri kamili au mawaziri wasaidizi.

Wengine walikuwa ni Charity Ngilu (Maji na Unyunyuzaji ), Sally Kosgei (Elimu ya Juu, Sayansi na Tekinolojia), Martha Karua (Haki , Uwiano wa Kitaifa na Masuala ya Katiba), Naomi Shaban (Mipango Maalumu) Esther Murugi Mathenge ( Jinsia na Masuala ya Watoto) na Beth Mugo (Afya ya Umma na Usafi).

Kwa vile hakuwa na uzoefu katika siasa na usimamizi, Sambili alikuwa na wakati mgumu katika kusimamia wizara ya Michezo na Masuala ya Vijana. Mnamo Agosti 2010, Rais alimhamishia Sambili katika Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki.

Baada ya muda mfupi, alipatiwa majukumu mengine akiwa kaimu- yale ya waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Tekinolojia- kufuatia kusimamishwa kwa William Ruto kutoka Baraza la Mawaziri kuhusiana na madai ya ufisadi. Ilikuwa ni kupanda na kupanda cheo kwa Sambili, mwanamke wa kwanza kutoka jamii ya Tugen kuwa mbunge na waziri.

Kwamba alishikilia nyadhifa mbili za uwaziri wakati mmoja ni ushahidi kwamba Rais na mshirika wake katika serikali ya muungano walikuwa wakimwamini na uwezo wake kama kiongozi.

Licha ya utendaji wake bora katika wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki, Sambili alijipata katika vita kati ya mahasimu wa kisiasa Raila Odinga na William Ruto na chembilecho wahenga, ndovu wanapopigana, ni nyasi huumia. Hivyo ndivyo aliondolewa katika Baraza la Mawaziri mnamo Agosti 2011.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Atwoli sasa aponda Uhuru akijipendekeza...

Mlipuko wa Kolera Tana River wahangaisha wakazi 10...

T L