• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 2:08 PM
WALIOBOBEA: Soita aliifaulisha miradi mingi ya makao katika enzi ya Kibaki

WALIOBOBEA: Soita aliifaulisha miradi mingi ya makao katika enzi ya Kibaki

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

PETER Soita Shitanda alikuwa kile ambacho waziri katika serikali ya Rais Mwai Kibaki alipaswa kuwa.

Kama mkubwa wake, alipenda kazi yake na alijua kuifanya.

Na kama Rais aliyemteua, katika chochote alichofanya, maisha ya watu alioteuliwa kuhudumia hayakuwa na budi kunufaika na kubadilika milele.

Mojawapo ya kumbukumbu zinazohusishwa na utawala wa Kibaki ni miradi ya maendeleo ya miundomsingi nchini ambayo ilikuwa imetelekezwa kwa miongo mingi na kama waziri wa makao, Soita Shitanda alihusika katika mabadiliko hayo yote na leo, miradi ya nyumba iliyoanzishwa na kutekelezwa na utawala wa Kibaki inadhihirisha kumbukumbu itakayodumu.

Shitanda aliyezaliwa 1959, alisomea shule ya msingi ya Tande kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Malava ambapo alichaguliwa kiranja.

Baada ya elimu yake ya sekondari, aliondoka Malava kujiunga na Kenya Polytechnic kabla ya kujiunga na Strathmore University kusomea uhasibu.

Baada ya kuhitimu Strathmore, Shitanda aliendeleza masomo yake Amerika kwa miaka mitatu kati ya 1993 na 1996. Lakini alipokuwa akiendelea na masomo yake, Shitanda alikuwa ameonja serikali. Akiwa Strathmore, Shitanda alifanya kazi katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Baada ya mwaka mmoja akifanya kazi katika afisi hiyo alihamia Wizara ya Fedha.

Wakati huo alikuwa ametumiwa jumbe kutoka Malava kuleta damu mpya katika siasa za eneo hilo. Wazee walimwendea mwana wa eneo lao aliyefanikiwa mbali na nyumbani.

Katika ngazi ya kitaifa, siasa zilikuwa zikibadilika pia. Wapigakura walitaka damu mpya na mawazo mapya. Vyama vipya vya kisiasa vilikuwa vimeundwa. Shitanda alisoma hali ya nchi.

Kenya ilifanya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka wa 1992 ambao Rais Daniel Moi aliyekuwa mamlakani alishinda.

Lakini kundi la wanasiasa, wafanyabiashara na hata maafisa wa serikali walikuwa wameng’amua hali ya baadaye ingebadilika.

Na kuelekea mwisho wa mwaka wa 1997, Shitanda aliacha wadhifa wake katika Investment Promotion Centre na kujiunga na bahari ya siasa ambayo wakati huo ilikuwa imejaa papa na nyangumi na akavutiwa na ilivyokuwa.

Kwake, bahari ya siasa haikuwa baridi wala yenye joto sana. Alichaguliwa mbunge wa Malava alilowakilisha kwa miaka 15.

Mwaka wa 2002 aliteuliwa waziri msaidizi katika Afisi ya Rais baada ya Kibaki kuingia mamlakani. Mwaka wa 2007, Shitanda alisajili chama cha kisiasa cha New Ford Kenya, na kuwa kiongozi wake nchi ilipokuwa ikikaribia kufanya uchaguzi.

Katika uchaguzi uliokumbwa na ghasia, chama chake kilishinda viti viwili – kimoja chake cha Malava na cha Boni Khalwale kama mbunge wa Ikolomani. Kibaki alimteua tena waziri wa Nyumba.

Mnamo Oktoba 12, 2012, wawili hao walizindua mojawapo ya miradi mikubwa ya nyumba katika mtaa wa Ngara.

Katika uchaguzi mkuu wa 2013, aligombea ugavana kaunti ya Kakamega na akashindwa na Wycliffe Oparanya. Shitanda alifariki dunia mnamo Mei 24, 2016 katika Nairobi Hospital baada ya kuugua maradhi ya figo kwa muda.

  • Tags

You can share this post!

DARUBINI YA WIKI, Januari 29, 2023  

JAMVI LA SIASA: Maasi ya Raila ni ‘moto wa...

T L