• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Wasanii mashuhuri waliofariki 2020 hivyo kuacha pengo kubwa katika fasihi yakiwemo majukwaa ya utunzi na ulumbi wa mashairi

Wasanii mashuhuri waliofariki 2020 hivyo kuacha pengo kubwa katika fasihi yakiwemo majukwaa ya utunzi na ulumbi wa mashairi

NA HASSAN MUCHAI

MWAKA 2020 tulipoteza watu mashuhuri nchini na mataifa ya kigeni.

Jukwaa la ushairi na Kiswahili kwa jumla halikuachwa nyuma. Kuanzia mwanzo wa mwaka 2020, kilikuwa ni kilio baada ya kilio. Tulianza na kifo cha Abdallah Shamte, Ken Walibora, Abdallah Mwasimba, Sudi Kigamba na mwisho Kombo Mataka Salim – Msijumu.

ABDALLAH ALI SHAMTE (1948-Februali 9, 2020)

Abdallah Ali Shamte aliyejulikana kwa lakabu ‘Mtumwa wa Mungu’ alifariki dunia Februari 9, 2020 akiwa na miaka 72, baada ya kuugua kwa muda mrefu. Mwili wake uliswaliwa masjid kwa-Shibu na kuzikwa maziara ya Kikowani.

Kifo cha Shamte kilikuwa cha kwanza mwaka jana na kiliacha pengo kubwa katika jukwaa la ushairi. Shamte alikuwa mshairi sugu katika gazeti hili kuanzia miaka ya 70. Pia alisikika sana kupitia kipindi cha mashairi – KBC Radio.

Shamte alikuwa ‘mtu wa watu’. Washairi wengi kutoka maeneo ya bara na pwani hawakukosa kufika nyumbani kwake Mwembe-Kuku kumsabahi , kumjulia hali na kupata mawili au matatu kutoka kwake. Alisifia ushairi wa kale na kila mara kumtaja mjomba wake Aziz Abdallah Kiwilo (Nyundo ya chuma) kama mwalimu wake wa kwanza.

Alikuwa mlumbi stadi na mtunzi asiyechelea kondo. Mapema miaka ya 70, kulitokea ushindani mkali baina ya washairi wa Tanga na Mombasa. Kutokana na jinsi alivojizatiti kulumbana, alipokea mwaliko kutoka kwa watoto wa Shaban Roberts, Iqbar na Hussein kutembea nyumbani kwao Tanga. Alikaa huko kwa siku mbili na kupata nafasi ya kuzuru kaburi la baba yao.

Shamte alizaliwa mtaa wa Mwembe Kuku, Mvita Mwaka 1948. Alipata masomo yake kutoka Arab School (sasa Serani Boys). Alijiunga na Arab Secondary school (sasa Khamis Secondary School) kabla ya kuhamia Taasisi ya Lumumba jijini Dar es Salaam, Tanzania kwa masomo ya kitaaluma.

KEN WALIBORA (Jan 6, 1965- Aprili 10, 2020)

Habari za Kifo cha Ken Walibora kilichotokea Aprili 10, 2020 zilitetemesha jukwaa la lugha ya Kiswahili. Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa Ken alifariki baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabara ya Landhies, jijini Nairobi.

Mwili wake ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kenyatta siku tano baada ya kuripotiwa kutoweka.

Mara tu baada ya habari za kifo chake kutangazwa, viongozi wengi mashuhuri akiwemo Rais Kenyatta walituma risala zao za rambirambi kwa jamaa, marafiki na wapenzi wa Kiswahili baada ya kumpoteza shujaa huyo aliyepigania kutambuliwa kwa lugha ya Kiswahili nchini, Afrika Mashariki na bara Afrika kwa ujumla.

Ken alizaliwa Januari 6, 1965, Kaunti ya Bungoma. Baadaye familia yake ilihamia eneo la Bonde, Makutano ya Ngozi, Kaunti ya Trans Nzoia. Mama yake Bi Ruth Makali aliyezaliwa mwaka 1933 alifariki Februari 10, 1984 huku babake Mwalimu Peter W. Murefu aliyezaliwa 1928 akiaga dunia Juni 23, 2006.

Alianza masomo yake katika St Joseph Primary School kabla ya kuhamia Teremi, Suremi Secondary kisha Ole Kajiado na Koelel.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka 2004 kabla ya kuhamia Ohio University nchini Marekani kwa shahada ya uzamili. Alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Wisconsin Madison.

Ken alikuwa mwandishi mtajika wa vitabu vya Kiswahili. Kitabu chake cha Siku Njema kilimzolea sifa kedekede. Alikuwa mwanahabari na aliwahi kufanya kazi katika mashirika kadhaa kama vile KBC na NTV. Hadi wakati wa kifo chake alikuwa mfanyakazi katika Chuo Kikuu cha Riara jijini Nairobi.

ABDALLAH MWASIMBA (1937 – Julai 30, 2020)

Karibu kila mshairi aliyeinukia miaka ya 70 hadi 2020 anamtaja marehemu Abdallah Mwasimba kama aliyechochea ari yake kutaka kutunga mashairi. Abdallah aliyezaliwa mwaka 1937 alifariki mwezi Julai Mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 83. Mwasimba alizikwa kwenye makaburi ya waislamu ya Kariakoo, Nairobi.

Mwasimba alikuwa mtunzi na mghani stadi wa mashairi aliyeanza kazi hiyo miaka ya 50. Bali na ushairi, Mwasimba alikuwa mtunzi wa hadithi na michezo katika shirika la KBC. Akiwa na wasanii wengine kama vile Juma Mrisho, Lolani Kalu, marehemu Musa Stephene na wengineo, Mwasimba alishiriki nafasi kubwa kwenye kipindi cha mchezo wa wiki. Alikuwa na kipindi kingine Janja na janjaure kilichokuwa kikisikika kupitia Redio ya KBC.

Mwasimba alishiriki nafasi ya mbele kuwaenzi washairi na wapenzi wa Kiswahili. Atakumbukwa daima Mei 13, 2007 kwenye ile safari ya kumuenzi marehemu Mwalimu Mbega eneo la Matuu kwani alitumbuiza umma uliokuwa kwenye ziara hiyo kwa mashairi matamu. Mwasimba alikuwa na kipawa cha kunakili na kughani mashairi ya watunzi wa kale mathalan Shaaban Roberts na Muyaka Bin Hajji.

SUDI KIGAMBA (Agosti 6, 1961- Novemba 25, 2020)

Ingawa alikuwa amezaliwa na kukulia Tanga, Sudi alikuwa na ufuasi mkubwa nchini Kenya. Alikuwa muasisi wa malumbano ya Mbega na Chombo yaliyochukua muda wa miaka 7 kukamilika. Alifariki akiwa na umri wa miaka 59 jijini London, Novemba 25, 2020.

Mwili wake uliwasili katika uwanja wa J.K Nyerere jijini Dar es Salaam Alhamisi Desemba 10 na kusafirishwa hadi Madina Tanga siku hiyo. Maiti iliswaliwa msikiti wa Madina kabla ya hafla ya mazishi iliyofanyika Ijumaa Desemba 11 kijijini Chongoleani.

Sudi Kigamba alizaliwa Agosti 6, 1961 katika Kijijini Chongoleani Mkoa wa Tanga, Tanzania na kusomea shule ya msingi ya Chuma kabla ya kujiunga na Dodoma Secondary. Baadaye alisafiri hadi Taasisi ya Seki iliyoko Arusha alikojifunza somo la Uhasibu. Alibahatika kuajiriwa kazi na benki ya National & Commerce. Aliachana na kazi hiyo kutokana na mazingira duni ya kikazi na kuhamia Saudi Arabia na kurudi tena Tanga na hatimaye Uingereza hadi alipofariki.

Sudi alijifunza sanaa ya ushairi kutoka kwa babake marehemu Kigamba K. Lungo aliyezaliwa Tanga 1930. Mzee Lungo alikuwa mmoja wa washairi waliopata mafunzo yao kutoka kwa marehemu Ghulam Mwinyi Matano (maarufu Mwalimu Mwabondo). Isitoshe, Sudi aliwahi kumtaja nyanyake marehemu Tajiri Yakukumo aliyekuwa manju mahiri wa kuimba ngoma za kitamaduni kama kichocheo chake katika ushairi.

Alianza utunzi wa mashairi 1975. Mwalimu wake wa kwanza wa ushairi alikuwa rafiki wa babake Bw S.O Hijaz (ustadh stara) wa Mombasa. Baadaye aliiga utunzi wa Mwinyi Hatib Mohammed na marehemu Abdallah Baruwa. Utunzi wake ulikuwa ukipigwa msasa na Mwalim Hassan Mbega.

MSIJUMU (1953 Nov- 28, 2020)

Kombo Mataka Salim au Msijumu (kishairi Msijumu wa Sina Ngowa) alizaliwa 1953 eneo la Mwagosi, Changamwe, Kaunti ya Mombasa. Alisomea shule ya Mvita na New- Era.

Kipawa chake cha utunzi wa mashairi kilikuwa ni urithi toka kwa babake Mataka Bin Kibwana Kombo. Baadhi ya wanawe ambao wamemrithi ushairi ni pamoja na Bi Halima Kombo.

Ingawa Msijumu hakuwa akijulikana sana na washairi wa kizazi cha sasa, alikuwa mtunzi stadi aliyeogopewa na wengi wa makamo yake. Alikuwa akitunga na kutuma mashairi yake miaka ya 70, 80, 90 hadi 2020 lakini akaacha kutokana na jukwaa la ushairi kuingiliwa na karaha za matusi. Alishiriki ulumbi wa chakacha miaka ya 80.

Marehemu alianza utunzi wa mashairi mwaka 1972 na alikuwa mtunzi wa nyimbo za taarabu ambapo alikuwa na kikosi chake kwa jina Shani Musical Club.

Msijumu alikuwa katika msitari wa mbele kutunga na kumtumbiuza Hayati Rais Moi wakati wa utawala wa chama cha Kanu. Baadhi ya vibao alivyotoa ni pamoja na lolo, Mtu hali na kadhalika. Aliwahi kutunga pia kibao Harambee kilichovuma miaka ya nyuma.

Marehemu Msijumu alikuwa ameandika mswada Malimwengu na Ulimwengu alichotarajia kuchapisha kabla ya kifo chake kutokea. Baadhi ya washairi alioshirikiana nao kwa karibu sana ni Rajab Pilau, Abdallah Kizere, Abdallah Aziz Kiwilo, Hassan Mwalim Mbega, Abdallah Hajji Dhado, Hamis Abdallah Chombo na wengineo.

You can share this post!

Mke akaangwa kutema mume aliyefutwa

Wapiganaji waua 25 DRC mkesha wa mwaka mpya