• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
ZARAA: Jinsi ushirikiano kati ya serikali na sekta ya binafsi utakavyosaidia kuokoa mazao mabichi

ZARAA: Jinsi ushirikiano kati ya serikali na sekta ya binafsi utakavyosaidia kuokoa mazao mabichi

NA SAMMY WAWERU

MAZAO mabichi ya kilimo kuharibika na kuozea shambani na kwenye masoko, ni miongoni mwa changamoto ambazo washirika katika mtandao wa uzalishaji hupitia.

Katika mengi ya masoko nchini, kuanzia mseto wa matunda mbalimbali, mboga, viazi, na karoti, mazao mengine yakiwa katika hali bora huonekana yametupwa kwa kukosa wanunuzi.

Taswira hiyo si tofauti na mashambani, wengi wa wakulima wakiishia kuyapa mifugo.

Kero hiyo inachochewa na miundomsingi duni ya soko, mabroka wakitumia mwanya huo kukandamiza wakulima na wafanyibiashara – yaani wanaofikishia walaji mazao.

Kufuatia mikakati ya wadauhusika, huenda hali hiyo ikaangaziwa kupitia mpango wa serikali na sekta ya binafsi kuanzisha maghala ya mazao mabichi.

Waziri msaidizi (CAS), Wizara ya Kilimo, Lawrence Omuhaka amesema serikali kwa ushirikiano na mashirika ya sekta binafsi inaendeleza mjadala kufanikisha mpango huo.

“Tunalenga kuleta jukwaani wawekezaji kutoka sekta ya binafsi, serikali na wakulima tufanye kazi kwa pamoja kuhakikisha mazao hayapotei,” Omuhaka akasema.

Alisema hayo kwenye kikao kilichoandaliwa na wadau sekta ya kilimo, kilichoshirikisha idara za serikali na kibinafsi jijini Nairobi.

Mpango wa maghala ya mazao mabichi ya shambani, Omuhaka alisema utasaidia kudumisha usalama wa chakula na kuwapa motisha wakulima kuendelea kuzalisha.

“Isitoshe, hatua hiyo itawasaidia kupata muda kutafuta soko bora na lenye ushindani kwa sababu mazao yatakuwa salama kwenye ghala,” akaelezea.

Soko la Ngong, lililoko kiungani mwa jiji la Nairobi japo katika Kaunti ya Kajiado, ni miongoni mwa masoko nchini yaliyoboreshwa.

Naibu Gavana Kajiado, Bw Martin Moshisho akitembeza ujumbe wa wawakilishi Sudan Kusini, kukagua muundo wa Ngong Market. PICHA | SAMMY WAWERU

Aidha, limekumbatia mifumo ya kisasa kuhifadhi bidhaa za kilimo inayojumuisha majokofu na vyumba vyenye bairidi.

Muundo wake unaepushia wafanyibiashara hasara ya bidhaa kuharibika au kuoza.

“Soko la Ngong ni mfano wa masoko Kenya ambayo yanapaswa kuigwa kuafikia mjadala wa maghala,” ahimiza Meshack Malo, mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Muungano wa Umoja wa Kimataifa (FAO), nchi ya Sudan Kusini.

Soko hilo limetembelewa na baadhi ya magavana nchini na ujumbe wa wawakilishi Sudan Kusini, kukagua muundo wake.

Ni mpango ambao ukiigwa na kutekelezwa katika masoko Kenya, utaondolea wafanyibiashara hasara hatua ambayo itawachochea kununua mazao kwa wingi.

Itakuwa afueni kwa wakulima, washirika katika mtandao wa uzalishaji chakula nchini wanaobeba mzigo wa ukuzaji, kuanzia gharama ya juu ya pembejeo hadi mahangaiko kupata soko.

  • Tags

You can share this post!

Carlos Tevez astaafu kwenye ulingo wa soka

Awamu ya tatu ya Kazi Mtaani yazinduliwa nchini

T L