• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
UFUGAJI: Mfugaji anayekumbatia kilimo-mseto afurahia matunda ya juhudi zake

UFUGAJI: Mfugaji anayekumbatia kilimo-mseto afurahia matunda ya juhudi zake

NA PETER CHANGTOEK

KATIKA shamba lenye ukubwa wa ekari tatu katika eneo la Iviani, karibu na barabara ya Kangundo, Kaunti ya Machakos, mfugaji mmoja anachuma hela kwa kuendeleza ufugaji ambapo huwafuga sungura, kuku na kondoo.

“Nilianza kufanya shughuli za ufugaji wa sungura miaka mitatu iliyopita,” asema Stephen Mutuku, 42, ambaye pia huikuza mimea mbalimbali kama vile mipapai, mikomamanga, mihindi na mipera.

Mkulima huyo ana zaidi ya kuku 300, na huuza mayai kwa bei ya Sh10 kila moja.

Baadhi ya kuku wanaofugwa na Stephen Mutuku. PICHA | PETER CHANGTOEK

Yeye huwafuga kuku wa kienyeji na hukusanya mayai zaidi ya 50 kwa siku moja kutoka kwa kuku wanaotaga mayai.

“Shamba letu ni ekari tatu, lakini sisi huitumia sehemu ndogo ya shamba kuwafuga kuku na sungura,” adokeza mkulima huyo.

Vibanda ambavyo yeye huvitumia kuwafuga kuku vimejengwa kwa mbao na mabati.

Mkulima huyo, pamoja na mkewe, Pauline Ndunge, wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbalimbali za kilimo. Hata hivyo, anasisitiza kwamba, mkewe ndiye huwashughulikia kuku hao wa kienyeji mara nyingi.

“Niliutumia mtaji wa Sh5,000 kuanzisha shughuli za ufugaji wa kuku na sungura. Niliwanunua sungura watatu – wawili wa kike na mmoja wa kiume kwa Sh500 kila mmoja wakati nilipokuwa nikianza,” afichua Mutuku.

Mfugaji huyo anasema kwamba, huwalisha sungura wake kwa kutumia lishe aina ya hay.

Kwa sababu kuna nyasi na majani mbalimbali katika eneo hilo, Mutuku hukusanya majani ya mimea tofauti tofauti kuwalisha sungura wake.

Aidha, anasema kwamba, wao hutengeneza lishe ambazo hutumia kuwalisha kuku wao, na kuwafungulia ili wajitafutie lishe za ziada shambani.

Mutuku huwafuga sungura aina tofauti, mathalani; Californian White, New Zealand White, Chinchilla na Flemish giant.

“Huwauza sungura hao kwa Sh800-Sh1,500. Bei za sungura hutegemea jinsia yao, umri na uzani wao,” asema mfugaji huyo, ambaye pia huwachinja sungura kwa mujibu wa oda anazopata kutoka kwa baadhi ya wateja wake.

Aidha, huuza kuku wao kwa bei tofauti tofauti, kwa kutegemea jinsia, umri, uzani, miongoni mwa mambo kadhaa anayozingatia wakati anapowauza.

Mkulima huyo anasema kwamba, huuza vifaranga kuanzia Sh100, hususan kwa wale wateja wanaonuia kuwanunua kwa ajili ya kuwafuga.

Pia, huwauza kuku waliokomaa kuanzia Sh300.

Vilevile, huwafuga kondoo aina ya Dorper, ambapo huwaachilia kutembeatembea wakila nyasi na mimea mingine shambani.

Anaongeza kwamba, huwauza kondoo kwa bei kuanzia Sh5,000, ikitegemea umri na ukubwa wa kondoo.

Anasema kuwa, katika siku za usoni, anapania kupanua shughuli za kilimo, ili awe na sungura, kuku na kondoo wengi zaidi ili apate riziki zaidi.

Mutuku anaongeza kwamba, mbolea wanazopata kutoka kwa mifugo wanaofuga, hutumia katika ukuzaji wa mimea mbalimbali shambani.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Waongezea maembe thamani kuvutia soko na faida zaidi

Azuiliwa rumande akituhumiwa kumuua ‘babe’ wake

T L