• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
CHARLES WASONGA: Njaa: Ruto, Raila wasaidie nchi kutafuta suluhu upesi

CHARLES WASONGA: Njaa: Ruto, Raila wasaidie nchi kutafuta suluhu upesi

NA CHARLES WASONGA

KIBONZO kilichochapishwa katika ukurasa wa 12 kwenye gazeti la “Sunday Nation” toleo la Oktoba 30, 2022 kimeweka hali halisi inayoshuhudiwa nchini.

Kinaonyesha wazi jinsi viongozi wakuu serikalini na wale wa upinzani wanazungumzia masuala ambayo hayatoi suluhu, ya haraka, kwa matatizo ya njaa na ukame yanayowazonga zaidi ya Wakenya 4.5 milioni wakati huu.

Rais William Ruto amechorwa akikariri jinsi serikali yake imeanzisha mpango wa utoaji mbolea kwa bei nafuu kwa wakulima humu nchini ili wazalishe chakula kwa gharama nafuu.

Kwa upande mwingine kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga, amesawiriwa akiendeleza kauli mbiu ya kupigania mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bado anazongwa na machungu baada ya kupoteza katika kinyang’anyiro cha urais kilichofanyika Agosti 9.

Huku Dkt Ruto akitumia muda mwingi kuzungumzia mbolea ya bei nafuu na Bw Odinga akiendelea kulalamikia ushindi wake katika uchaguzi mkuu uliopita, mchoraji kibonzo hicho anamsawiri mwananchi wa kawaida aliyedhoofika kimwili kutokana na makali ya njaa.

Ujumbe ambao msanii huyu anapitisha kwa viongozi hawa wawili ni kwamba, Wakenya waliorauka alfajiri kuwapigia kura kwa wingi, wanateseka ilhali wao wanazungumzia masuala ambayo hayawasaidii sasa hivi.

Mpango wa serikali wa kuwauzia wakulima mbolea kwa bei ya Sh3, 500 japo ni bora ila ulianza wakati ambapo wakulima katika maeneo yanakozalisha mahindi kwa wingi walikuwa tayari wamepanda mazao.

Isitoshe, wengi wa wakulima ambao hupanda mahindi katika msimu wa mvua chache wa kati ya Septemba na Desemba walikuwa tayari wamepanda.

Baadhi yao walikuwa wamenunua mbolea ya upanzi ya bei ghali ya Sh6,500 kwa gunia la kilo 50, ambapo wanatarajia kuvuna mwishoni mwa Desemba 2022.

Kwa hivyo, kimsingi mpango huu ambao ulianzishwa na Serikali ya Dkt Ruto baada ya kuapishwa kwake mnamo Septemba 13, hautawafaidi Wakenya wakati huu kwa kusaidia kupunguza bei ya unga.

Nao mpango wa usambazaji wa chakula cha msaada kwa waathiriwa wa baa la njaa, haujapunguza makali ya changamoto hii kwani raia wengi bado wanalalama kwamba hawajapata msaada huo.

Wafugaji kutoka sehemu mbali mbali nchini pia wanalalamika kuwa wanapata hasara baada ya mifugo wao kufa kwa kukosa lishe na maji.

Kwa mfano, wafugaji katika kaunti ya Kajiado wanasema kuwa wao hulazimika kuuza ng’ombe wao kwa bei duni ya Sh500 kwani wamedhoofika zaidi.

Nadhani haya ndio masuala ambayo Dkt Ruto na wakuu katika serikali yake wanafaa kushughulikia kwa dharura wakati huu.

Naye Bw Odinga kama kiongozi wa upinzani anafaa kutekeleza wajibu wake wa kumsukuma Dkt Ruto kutatua tatizo hili la njaa badala ya kutumia muda mwingi kuwakumbusha Wakenya kuhusu jinsi IEBC ilivyochangia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Odinga atawafaa zaidi Wakenya 6.9 milioni waliopigia kura katika uchaguzi huo kwa kupigania haki yao ya kupata usaidizi kutoka kwa serikali iliyoko mamlakani wakati huu.

Kampeni yake ya sasa ya kushinikiza mageuzi katika IEBC au mageuzi ya Katiba, haziwafaa wafuasi wake kote nchini, ambao wengi wao wanakeketwa na njaa.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Wakenya wote waitikie wito wa kulipa ushuru...

Vihiga Boys ni wafalme wa raga ya Prescott Cup

T L