• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 3:19 PM
JURGEN NAMBEKA: Heko Mwadime kutimua wafisadi ila uozo unatisha

JURGEN NAMBEKA: Heko Mwadime kutimua wafisadi ila uozo unatisha

NA JURGEN NAMBEKA

GAVANA wa Kaunti ya Taita Taveta Bw Andrew Mwadime wiki iliyopita aliwatimua afisini maafisa wanne kwa madai ya ubadhirifu wa fedha. Kati ya maafisa hao, wawili wanasemekana kuwa washauri wakuu wa gavana huyo.

Kulingana na barua aliyotuma gavana kuwasimamisha kazi kwa muda usiojulikana maafisa hao, alieleza kuwa walifuja pesa zilizotengwa kuandaa sherehe za maadhimisho ya Vita vya Dunia ambazo zilifanyika mnamo 2021.

Taarifa zinaeleza kuwa umma ulilalamikia suala hilo, na kumsukuma gavana kuanzisha uchunguzi.

Watoa huduma mbalimbali walijitokeza kupinga kujihusisha kwao na kutoa huduma mbali mbali katika sherehe hizo.

Wengi walidai kuwa wahusika walitumia majina yao katika risiti walizogushi ili kujifaidi wenyewe. Haya yakijiri kuna mambo yanajitokeza bayana.

Huenda Bw Mwadime akawa amewagundua washukiwa wa ubadhirifu na kuwachochea magavana wengine wa Pwani kufanya hivyo kwa manufaa ya wakazi wa kaunti za Pwani.

Licha ya gavana huyo kuwasimamisha kazi hadi uchunguzi kukamilika, je ni hafla hiyo tu iliyotumika kufuja pesa?

Wakazi huenda wakaibua maswali mengi, kuhusu kutimuliwa huku kwa wafanyakazi hao ikibainika kuwa kati yao walikuwepo washauri wa gavana. Ila suala kuu ni kilichopelekea maafisa hao kujipata taabani wakitaka kujichumia zaidi.

Kulingana na malalamishi ya magavana kuhusu kuchelewa kwa mgao wa fedha kutoka kwa serikali kuu, kuna uwezekano kuwa maafisa hao wa kaunti walikuwa wamekaa kwa muda bila kupokea mshahara.

Katika kuchelewa kwa mishahara hii, inakuwa vigumu kwa wao kuepuka majaribu ya kujitafutia kwa njia mbadala.

Licha ya kuwa sio halali, endapo maafisa hao wangelipwa mishahara kwa muda na ipaswavyo, wangekuwa waadilifu zaidi kazini.

Maswali haya yanaashiria pia kuwa, huenda kuna mengi zaidi ambayo hadi kwa sasa hayajajulikana kwa umma.

Uozo uliopo ndani ya serikali za kaunti unawapa wasiwasi Wakenya, kila wanapokwenda kupanga foleni ya kupiga kura.

Ni dhihaka kwa wapiga kura wanapofahamu waliyemwamini hawathamini kabisa na kuona mali yao ikiporwa. Kwa Bw Mwadime ambaye aliamua sakata hiyo ya Sh 4 milioni haitafichwa chini ya zulia , ni mfano bora kwa magavana wengine.

Bw Mwadime aliamua hatofumbia jicho hujuma hiyo, licha ya kuwa na usuhuba wa karibu na maafisa hao.

Ni chagamoto kwa magavana na wafanyakazi wengine, ambao wakipata nafasi ya kutumikia umma huingia mle kupora fedha za umma. Ni ombi langu kuwa, isiwe tu ni kiini macho kwa wananchi. Gavana asiwe amewatimua hawa wanne ilhali kuna maafisa wengine wanaouma na kupuliza ndani ya serikali.

Magavana wenza waige mfano wa Bw Mwadime kwa manufaa ya wakazi waliowachagua. Fursa ni ya kutumikia wananchi na siyo kupora mali yao.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi wachezaji wa kigeni walivyong’aa mashindano ya...

Sadio Mane kuadhibiwa kwa kumlima ngumi Leroy Sane

T L