• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Vyama vikubwa visitumie hila kuzuia uhamaji

TAHARIRI: Vyama vikubwa visitumie hila kuzuia uhamaji

KITENGO cha UHARIRI

RIPOTI zimeibuka kuwa, baadhi ya vyama vikubwa vimepanga kuchelewesha kura za mchujo kimakusudi ili wale watakaoshindwa wasihamie kwingine. Hizo ni habari za kutisha kwa kila anayekumbatia mfumo wa utawala wa demokrasia.

Taifa hili limekomaa kidemokrasia ikilinganishwa na miaka iliyopita kupitia uwepo wa vyama vingi vya kisiasa na vile vile, katiba inayoruhusu wanasiasa kuwania nyadhifa bila kutegemea vyama.Vyama vikubwa vilipata pigo katika chaguzi zilizopita kwa vile wanasiasa waliodhulumiwa katika mchujo waliamua kuhamia kwingine au kuwa wagombeaji huru.

Katika maeneo mengi, vyama vikubwa vilipoteza nafasi zao kwa kuwa walioshinda ni wale walionyimwa tikiti.Hali hii ilitarajiwa kuwafumbua macho viongozi na maafisa wakuu wa vyama vikubwa.Ingetarajiwa wangeona jinsi wananchi katika maeneo mbalimbali wameanza kufunguka macho na hawataki tena siasa za kuchagua viongozi kwa misingi ya vyama.

Hii ingewapa nafasi wakuu wa vyama vikubwa kurekebisha mifumo na taratibu zao za ndani ili kuhakikisha tikiti inaendea kiongozi ambaye wananchi wanamtaka.Hata hivyo, ripoti zilizoibuka kuhusu uwezekano wa baadhi ya vyama kuchelewesha kura ya mchujo ili watakaohisi wamedhulumiwa wasipate nafasi ya kuhama, ni sawa na kurudisha nchi katika enzi ya mfumo wa chama kimoja.

Yamkini vyama hivyo tayari vimebashiri kuwa kutakuwa na ukandamizaji katika utoaji wa tikiti za kuwania viti.Ikiwa viongozi wa vyama wana hakika kuwa tikiti itaendea wanasiasa ambao wananchi wanataka, basi hakungekuwa na njama hizi tunazosikia ambazo zinalenga kuwashika mateka wawaniaji.

Kumekuwa na madai ulaghai katika utoaji wa tikiti za kuwania nyadhifa tofauti za kisiasa nchini.Mbinu haramu kama vile utoaji hongo kwa maafisa wanaohusika katika kukabidhi wagombeaji tikiti hutajwa mara kwa mara.Isitoshe, vyama vya kisiasa vinafaa kutilia maanani hitaji la kuchunguza maadili ya wagombeaji wanaoruhusiwa kushiriki katika mchujo.

Huku msisimko kuhusu uchaguzi ujao ukizidi kutanda, wanasiasa wengi tayari wameonyesha dalili kuhusu vyama ambavyo wamenuia kutumia kuwania viti tofauti.Vyama hivyo vinawajibika kupiga msasa wawaniaji kwa ushirikiano na IEBC kwa lengo la kuondoa wanasiasa ambao uadilifu wao ni wa kutiliwa shaka.

You can share this post!

Majangili wapigwa risasi na wanajeshi waliolenga wezi

Polisi walia mishahara yao kupunguzwa

T L