• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Tumakinike tusichochee ghasia kama zilizozuka 2007

KINYUA BIN KING’ORI: Tumakinike tusichochee ghasia kama zilizozuka 2007

Na KINYUA BIN KINGORI

KIPINDI hiki cha siasa tusipokuwa makini huenda uchaguzi mkuu wa 2022 ukachochea ghasia na maonevu ya kikabila.

Makundi ya wanasiasa na wafanyabiashara matajiri kutoka eneo la Mlima Kenya wanaojiita wanachama wa wakfu wa Mlima Kenya (MKF), wamejitokeza kuwafanyia mahojiano kinara wa chama cha ODM Raila odinga na viongozi wa muungano wa OKA ili wajue ni kiongozi yupi bora miongoni mwao ambaye wataunga mkono kugombea urais kwa masharti makali ya kulindwa kwa mali yao akiwa Rais.

Je, kwa nini baadhi ya matajiri wa eneo moja wajitokeze hadharani kusuka mikakati katika siasa kwenye uchaguzi ujao?

Kwani kuna mali yao waliyopata kupitia njia haramu ndipo wanahofia kupoteza ikiwa kiongozi mwingine ataingia mamlakani bila ushawishi wao?

Je, wanajua kikatiba ni wajibu wa kiongozi kulinda mali na maslahi ya Wakenya wote bila kujali rangi, kabila au mrengo wa kisiasa?

Ikiwa nia yao ni njema mbona wamebagua wawaniaji wengine?

Mikakati ya kundi la MKF pekee haiwezi kupiga jeki waziri huyo mkuu wa zamani, au Kalonzo Musyoka ama Musalia Mudavadi kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta anayestaafu mwaka 2022.

Hivyo, wanasiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wasihadaike kuwa wanaweza kufaulu kuwa viongozi kwa kutegemea kundi fulani kuchaguliwa kuwa Rais wa taifa hili.

Kundi hilo linafaa kutupa wasiwasi kama taifa, maana huenda jamii nyinginezo ziwaige na kuunda makundi yao nao kwa lengo la kuunga mkono kiongozi atakayesaidia kulinda maslahi ya watu wao.

Wanasiasa wengi hasa wanaoshukiwa kuwa fisadi watatumia msimu wa siasa za urithi kupanga mikakati ambayo itawasaidia kuepuka kunaswa na kushtakiwa na Tume ya Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kwa mashtaka ya ufisadi ikiwa kiongozi wanayepigia debe atachaguliwa kuwa rais.

Mikakati ambayo tunafaa kuunga mkono inafaa iwe yenye kuzingatia uwazi, usawa na utaifa wetu, ambayo itaunganisha Wakenya wote na maslahi yao.

Makundi yanayojitwika majukumu ya kuamua kiongozi anayestahili kuungwa mkono na kundi fulani au jamii fulani yanafaa kupuuzwa maana yanaweza kuchochea hali ya wananchi kutoamini matokeo ya Tume Uchaguzi (IEBC) kwa kushuku mshindi amependelewa.

Mgawanyiko wa kisiasa unaoshuhudiwa Mlimani kwa sasa umechochewa na kuchipuka kwa kundi hilo.

Kuna baadhi ya wanasiasa wanaodai kundi hilo halina umaarufu mwingi mashinani na wananchi ndio wanajua mgombezi watakayemchagua kuwa rais 2022.

Itakuwa bora ikiwa Wakenya watapewa heshima na nafasi ya kuwapiga darubini wanasiasa wenye azma ya kuwania urais 2022, na kuchagua bila shinikizo wala kutiwa hofu na propaganda kisiasa.

Hii, ndiyo njia mwafaka ya kuzuia kuzuka kwa ghasia na machafuko kama yaliyolikumba taifa hili katika uchaguzi wa 2007.

  • Tags

You can share this post!

Jaji mkuu kuapisha majaji sita endapo Rais Uhuru Kenyatta...

Man-United watoka nyuma na kuzamisha chombo cha Atalanta...

T L