• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Man-United watoka nyuma na kuzamisha chombo cha Atalanta ugani Old Trafford

Man-United watoka nyuma na kuzamisha chombo cha Atalanta ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili katika mchuano ulioshuhudia waajiri wake Manchester United wakitoka nyuma na kukomoa Atalanta ya Italia 3-2 katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumatano usiku ugani Old Trafford.

Masogora wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walizomewa na mashabiki mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya utepetevu wao kuruhusu wageni kujiweka kifua mbele kwa mabao 2-0 kupitia Mario Pasalic na Merih Demiral waliocheka na nyavu katika dakika za 15 na 28 mtawalia.

Hata hivyo, kulishuhudiwa mabadiliko makubwa ya hisia miongoni mwa mashabiki wa Man-United katika kipindi cha pili baada ya Marcus Rashford kurejesha waajiri wake mchezoni katika dakika ya 53. Bao hilo liliwapa Man-United motisha ya kuvamia Atalanta na juhudi zao zikazaa matunda katika dakika ya 75 nahodha Harry Maguire alipojaza kimiani krosi kutoka kwa Edinson Cavani.

Sawa na alivyofanya dhidi ya Villarreal wiki tatu zilizopita, Ronaldo ndiye alishindia Man-United mechi dhidi ya Atalanta kwa kupachika wavuni bao la tatu katika dakika ya 81. Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus aliruka juu na kukamilisha krosi ya Luke Shaw kwa kichwa.

Ushindi wa Man-United uliwapaisha hadi kileleni mwa Kundi F kwa alama sita, mbili zaidi kuliko Atalanta na Villarreal. Young Boys inashikilia nafasi ya nne kwa pointi tatu.

Mechi hiyo ilikuwa ya tano kati ya saba zilizopita chini ya kocha Solskjaer kwa Man-United kujipata nyuma katika kipute cha UEFA.

Man-United wangali na ratiba ngumu mbele yao ikizingatiwa kwamba watavaana na Liverpool katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 24, 2021 uwanjani Old Trafford kabla ya kuvaana na Tottenham Hotspur ligini. Baada ya kurudiana na Atalanta ugenini katika UEFA mnamo Novemba 2, Man-United watapepetana na Manchester City siku nne baadaye katika EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Tumakinike tusichochee ghasia...

Walevi wapumua

T L