• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Wakenya wawe na mazoea ya kupima maradhi

TAHARIRI: Wakenya wawe na mazoea ya kupima maradhi

Na MHARIRI

TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa wiki hii, zinaonyesha ugonjwa wa saratani bado ni hatari kwa mamilioni ya watu.

Ingawa ulimwengu unakumbwa na aina mpya ya corona (Omicron), bado ugonjwa wa kansa unaua wengi, hasa familia zisizojiweza kifedha.

Ni ugonjwa hatari ambao usipogunduliwa mapema, husababisha familia kutumbukia katika umasikini, na mwishowe ni mauti.

Kulingana na WHO, hapa Kenya kansa ya njia ya uzazi na ile ya utumbo ndizo zinazoongoza.

Pia kuna kansa za ubongo, ngozi, damu, mifupa na kadhalika.Maradhi ya kansa yanaweza kutibiwa kwa gharama ndogo iwapo mgonjwa atafika hospitalini yakiwa katika hatua za mwanzo.

Kansa huanza sehemu moja na kusambaa pole pole hadi kuzagaa mwili mzima.

Watu wengi wanaotembelea hospitali hapa Kenya huwa wameanza kuhisi athari za ugonjwa huo. Hapo, madaktari huwa hawawezi kuutibu tena.

Kinachofanywa ni wagonjwa kuandikiwa safari za kutembelea hospitali mara kadhaa kwa mwezi.

Tiba hiyo kupitia miale huitwa radiotherapy na pia kuna chemotherapy. Hizi ni tiba zinazotumia miale maalumu kuchoma kansa hiyo.

Gharama yake si rahisi kwa yeyote. Mbali na kupitia shughuli hiyo, wagonjwa hutakiwa kutumia maelfu kununua dawa. Lakini kufanya hivyo si hakikishe kuwa mtu atapona.

Takwimu zinaonyesha kwa mfano mwaka 2019, kati ya wagonjwa 4,800 waliokuwa wakitibiwa, ni 29 pekee ambao hawakufa.

Huu ni ugonjwa unaoweza kudhibitiwa mapema iwapo mtu atajiwasilisha hospitalini kupimwa.

Lakini pia mtu anaweza kuepuka kupata kansa kwa kuzingatia mambo rahisi.

Kwanza ni kuishi katika mazingira safi. Iwapo ni nyumba, kila mara madirisha yawe wazi ili kuingiza hewa safi. Kusiwe na kemikali kama zile za kuua wadudu mashambani kwa muda mrefu.

Uvutaji sigara na uvutaji hewa ya mvutaji pia ni mambo yanayochangia zaidi ya nusu ya visa vya kansa.

Kilicho muhimu kwa watu ni kupimwa mara kwa mara na kujiepusha na tabia zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Utumizi wa simu au kompyuta kwa muda mrefu bila ya kufanya mazoezi ni hatari. Watoto kwa watu wazima kwenye karne hii ya mitandao ya WhtasApp, TikTok na mingine inayoshughulisha kwa muda mrefu, wanapaswa kujilazimisha kufanya mazoezi ya viungo.

Mara kwa mara serikali na mashirika ya kibinafsi huandaa kambi za matibabu ya bure.

Wakenya wanapaswa kufanya mazoea ya kuhudhuria matibabu hayo, ili wawe wakipimwa kama wana maradhi yanayohitaji tiba ya haraka au la.

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Natamani nipewe kazi ya uwaziri ninyoroshe...

Unesco yatambua muziki wa rhumba kama turathi kuu

T L