• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Afisa adai baadhi ya wachezaji wa Mathare United walihusika katika upangaji matokeo ya mechi za timu

Afisa adai baadhi ya wachezaji wa Mathare United walihusika katika upangaji matokeo ya mechi za timu

NA JOHN ASHIHUNDU

AFISA Mkuu Mtendaji wa klabu ya Mathare United Jecton Obure, amedai kwamba baadhi ya wachezaji walichangia katika kushuka timu hiyo hadi daraja la Supa Ligi (NSL), huku akidai kwamba wachezaji hao walihongwa kuuza mechi za Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) msimu uliopita.

Akihojiwa juma hili kueleza kuhusu maandalizi yao ya msimu ujao, Obure alikiri kwamba timu hiyo ilikabiliwa na hali ngumu ya kifedha, lakini akasisitiza kwamba baadhi ya wachezaji kikosini walitumiwa kupanga matokeo ya mechi na kusababisha timu hiyo kuteremshwa ngazi.

Alisema itakuwa bora zaidi iwapo FKF itafanya kazi karibu na wote wanaohusika, ikiwa ni pamoja na vyombo vya usalama nchini na kimataifa, sio tu kusaidia katika mashtaka ya washukiwa waliotajwa, bali katika jitihada za kulenga uadilifu wa soka nchini kwa jumla.

Mwezi Novemba 2022 kabla ya msimu uliomalizika kuanza FKF kwa usaidizi wa Shirikisho la Kimataifa la soka (FIFA) iliandaa warsha ya mafunzo kwa wasimamizi wa mechi na viongozi wa klabu za ligi kuu ambapo Mkuu wa Kitengo cha Maadili katika shirikisho la soka nchini, Mike Kamune alitao mafunzo na kuwajulisha wahusika katika kugundua, kuzuia na kuripoti shughuli za udanganyifu, huku akitoa nambari maalum ya simu ya 0790115228 kuripoti visa hivyo.

Miezi mitatu awali, klabu ya Mathare iliwapiga marufuku mchezaji Lennox Ogutu na Alphonce Ndonye, mwezi mmoja baada ya FKF kuwapiga marufuku wachezaji 14 na makocha wawili kufuatia madai kwamba walihusika katika upangaji wa matokeo.

Miongoni mwa waliofungiwa ni sita kutoka Zoo Kericho ambayo ilitolewa kwenye ligi kuu mnamoi 2021. Februari 2020, FIFA ilimpiga marufuku ya maisha mchezaji mmoja pamoja na waamuzi watano kutokana na madai ya kuhusika katika kupanga matokeo ya mechi.

Mathare waliteremshwa ngazi baada ya kumaliza katika nafasi ya 17 msimu uliopita wa 2022/2023 baada ya kushindi mara nane pekee katika mechi 34.

“Wakati fulani tuliendelea kuandikisha matokeo mazuri, lakini ghafla tukaanza kupoteza mechi kiurahisi. Tulikuwa na kikosi imara cha kuokoa timu, lakini njama za hongo zilituponza.”

“Njama za wachezaji kutumiwa kuuza mechi zilkianza wakati wa Kamati ya Mpito ilipochukuwa usukani msimu wa 2021/2022, kwa sababu wachezaji walifahamu hakuna hakuna hatua wangechukuliwa. Mpango huu ulihusisha watu wengi, kuanzia kwa wachezaji, maafisa wa klabu pamoja na waamuzi wa mechi hizo,” aliongeza Obure.

“Tunataka sheria ipitishwe Bungeni ili yeyote atakayepatikana kuhusika katika hali kama hii akamatwe na kushtakiwa,” alisema.

“Niliangalia baadhi ya mabao tuliofungwa na kushangazwa zaidi. Kwa mfano, wachezaji waliofaa kulinda eneo la hatari, wakati mwingine walionekana walikosa kukabiliana na washambuliaji huku wengine wakihepa mpira ili uingie.”

“Wakati huu tunajiandaa kushiriki mechi za NSL, tungependa sheri ipitishwe ya kukabili tabia hii ya kutafuta pesa kwa mkato, wakati timu ikiumia,” aliongeza afisa huyo aliyesema Mathare inajipanga vyema ili irudi kwenye ligi kuu haraka.

  • Tags

You can share this post!

Ruto akosolewa kupeana hatimiliki kwa wanahisa Embakasi...

Hatima ya Junior Starlets kushiriki dimba la CECAFA...

T L