• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
Ruto akosolewa kupeana hatimiliki kwa wanahisa Embakasi Ranching

Ruto akosolewa kupeana hatimiliki kwa wanahisa Embakasi Ranching

NA MWANGI MUIRURI

WAKURUGENZI wa mradi wa mashamba ya Embakasi sasa wamemkosoa Rais William Ruto kwa madai ya kukiuka maagizo ya mahakama kuhusu utozaji wa hatimiliki kwa wanahisa.

Mwenyekiti wa Embakasi Ranching Bw James Njoroge pamoja na wakili wa wanahisa Bw Timothy Kariuki walilalamika kuwa wiki jana Rais Ruto alikiuka sheria kwa kutoa baadhi ya hatimiliki hizo.

Wawili hao walitoa agizo la mahakama ambalo Jaji Philomena Mwilu ambaye kwa sasa ndiye Naibu wa Jaji Mkuu aliagiza utoaji wa hatimiliki katika kampuni hiyo uahirishwe hadi kesi iliyokuwa imewasilishwa ya kupinga isikilizwe na iamuliwe.

“Kesi hiyo imenakiliwa katika sajili ya mahakama kama kesi ya kibiashara nambari 395 ya mwaka wa 2011 iliyowasilishwa na Bi Josephine Njeri Gakami,” akasema Bw Kariuki.

Bi Gakami alikuwa amewasilisha malalamiko kwamba sajili ya wanahisa ilikuwa imepenyezwa wanahisa bandia na ambao walijumuisha wakubwa katika vitengo vya serikali, maafisa wa usalama wakiwa ndio wengi.

Katika mchakato wa kutoa hatimiliki, sajili hiyo ya wanahisa ikiwa na wanyakuzi hao, akalilia mahakama, ilikuwa ni sawa na kuhalalisha wizi na unyakuzi.

Katika uamuzi wake wa Februari 15, 2012, Jaji Mwilu alipiga breki utoaji wa hatimiliki na akaamrisha msajili wa mashamba pamoja na Wakili Mkuu wa serikali pamoja na wafanyakazi wao wote wasitoe hatimiliki hata moja kwa mwanahisa yeyote.

Agizo la Jaji Mwilu liliongeza kuwa “ukiukaji wa agizo hili utakuwa na lawama ya kisheria dhidi ya yeyote atakayethubutu”.

Na kwa kuwa kesi hiyo haijawahi kuamuliwa, Bw Njoroge na Bw Mwangi walihoji hatua ya Rais kufika katika makao ya kampuni hiyo na kuzindua hafla ya upeanaji hatimiliki.

Walisema kwamba kwa sasa kuna malalamishi 15,000 ya mashamba ya wanahisa kunyakuliwa na hatua ya Rais inaidhinisha wizi huo. Walisema kwamba watawasilisha malalamishi yao mahakamani ili hatua hiyo ya Rais izomewe na iamuliwe kuwa haramu kwa kuwa kinyume na sheria.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Rais wa LSK ahimiza waandamanaji wafuate sheria

Afisa adai baadhi ya wachezaji wa Mathare United walihusika...

T L