• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Arsenal wasubiri hadi dakika za mwisho kuzamisha chombo cha Aston Villa katika EPL

Arsenal wasubiri hadi dakika za mwisho kuzamisha chombo cha Aston Villa katika EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliweka kando maruerue ya kutoshinda mechi nne mfululizo na kutoa ishara ya jinsi walivyo tayari kutwaa ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kukomoa Aston Villa 4-2 uwanjani Villa Park.

Vijana wa kocha Mikel Arteta walipachika wavuni mabao mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Gabriel Martinelli na kipa Emiliano Martinez aliyejifunga.

Ollie Watkins aliweka Villa kifua mbele kunako dakika ya tano kabla ya Bukayo Saka kusawazisha dakika 11 baadaye. Ingawa Philippe Coutinho alirejesha Villa mchezoni katika dakika ya 31, juhudi zake zilizimwa na Oleksandr Zinchenko kunako dakika ya 61.

Sawa na Villa waliopoteza pambano lao la awali ligini kwa 3-1 dhidi ya Manchester City ugani Etihad, Arsenal pia walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kukubali kichapo cha 3-1 kutoka kwa mabingwa hao watetezi wa EPL uwanjani Emirates.

Arsenal ambao sasa wanajivunia alama 54, wametandaza jumla ya michuano 23 ambapo wameshinda 17, kutoka sare mara tatu na kupoteza tatu. Tofauti na Man-City waliovaana jana na Nottingham Forest ugenini, Arsenal wana mechi moja zaidi ya akiba.

Chini ya Unai Emery ambaye ni mkufunzi wa zamani wa Arsenal, Villa sasa wamefungwa mabao 11 kutokana na michuano mitatu iliyopita ingawa wamefaulu kucheka na nyavu za wapinzani wao katika mechi 12 mfululizo za mashindano yote.

Villa wameokota mpira kimiani katika kila mojawapo ya mechi sita zilizopita za EPL nyumbani huku wakishinda pambano moja pekee katika kipindi hicho. Matokeo ya jana dhidi ya Arsenal yaliwaacha na alama 28 baada ya michuano 23.

Ushindi uliosajiliwa na Man-City ugani Emirates mnamo Jumatano uliendeleza ubabe wao dhidi ya Arsenal ambao sasa wamepoteza mechi 11 zilizopita dhidi ya miamba hao wa EPL.

Arsenal walijibwaga jana uwanjani wakipigiwa upatu wa kutojikwaa zaidi baada ya kutoshinda mechi tatu mfululizo ligini na kung’olewa na Man-City kwenye Kombe la FA. Kabla ya kubamizwa Jumatano usiku, walikuwa wametoshana nguvu na Brentford kwa sare ya 1-1 uwanjani Emirates na kucharazwa 1-0 na Everton ugenini.

Licha ya matokeo hayo duni, Arsenal wanaowania ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza tangu 2003-04, walitua Villa Park wakijivunia rekodi ya kufungwa mabao saba pekee kutokana na mechi zote za ugenini msimu huu.

Kikosi hicho ambacho pia hakijawahi kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) tangu 2016-17, kilipepeta Villa 1-0 ugenini msimu uliopita kabla ya kuvuna ushindi wa 2-1 ugani Emirates mwishoni mwa Agosti 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO  

  • Tags

You can share this post!

VITUKO: Sasa mrembo Ivana awinda penzi la Jesus huku kipusa...

Omanyala aomba serikali iweke mazulia Kasarani, Mombasa na...

T L