• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Omanyala aomba serikali iweke mazulia Kasarani, Mombasa na Kisumu kuinua talanta ya mbio fupi

Omanyala aomba serikali iweke mazulia Kasarani, Mombasa na Kisumu kuinua talanta ya mbio fupi

Na AYUMBA AYODI

BINGWA wa Jumuiya ya Madola mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala ameomba serikali iweke mazulia ya kukimbilia katika viwanja vya Mombasa na Kisumu ili kufanikisha ukuzaji wa talanta ya mbio fupi nchini.

Akizungumza baada ya kuwasili kutoka Ufaransa hapo Februari 17, afisa huyo wa polisi alisema kuwa maeneo hayo mawili yametoa talanta nzuri katika mbio fupi na kuongeza kuwa yana hali nzuri ya anga kwa matayarisho ya msimu mpya.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika mbio za 100m pia ameomba Halmashauri ya Kusimamia Viwanja nchini (Sports Kenya) kuweka zulia jipya la kufanyia mazoezi katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani kwa sababu lile liko limeharibika na si nzuri kwa mazoezi ya mbio fupi.

Omanyala, ambaye hufanyia mazoezi yake katika uwanja wa Kasarani, pia amesema kuwa serikali iwazie kutenga sehemu ya kuwakumbuka mashujaa katika kituo cha michezo cha Kasarani ili kusherehekea mashujaa wa kiume na pia kike kutoka Kenya.

“Kwa muda mchache nimekuwa mtimkaji wa kulipwa, nimeona tofauti katika mazingira ya kufanya mazoezi nilipozuru Bara Ulaya,” alitanguliza Omanyala aliyeimarisha rekodi yake kitaifa ya 60m za ukumbini mara mbili akitimka nchini Ufaransa.

“Naamini miji ya Mombasa na Kisumu inaweza kuwa mizuri kwa mazoezi ya wakimbiaji wa mbio fupi kwa hivyo natoa ombi hilo… Kitakuwa kitu kikubwa kabisa kwa wanariadha hapa Kenya viwanja hivyo vikipata vifaa hivyo,” alisema Omanyala baada ya kukaribishwa nchini kwa kuandaliwa kiamshakinywa na Sports Kenya kwa heshima yake katika hoteli ya Stadion, Kasarani.

Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Katibu wa Michezo Jonathan Mueke, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Michezo, Utalii na Utamaduni Dan Wanyama, Mwenyekiti wa Sports Kenya Charles Waithaka na Mkurugenzi Mkuu wa Sports Kenya Pius Metto.

Mueke na Wanyama waliapa kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na Omanyala, hasa kuwekea wakimbiaji zulia la kufanyia mazoezi.

“Ningependa sana kufanyia mazoezi Mombasa ama Kisumu kabla ya michezo ya Olimpiki mjini Paris mwaka ujao na hata baada ya michezo hiyo. Najua inawezekana na uongozi uliopo,” alisema Omanyala anayeshikilia rekodi za kitaifa za 60m (sekunde 6.54) na 100m (9.77).

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Arsenal wasubiri hadi dakika za mwisho kuzamisha chombo cha...

LSK yatisha kuishtaki serikali kwa kutuma jeshi katika...

T L