• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Barcelona wakomoa Valencia na kuweka hai matumaini ya kuibuka wafalme wa La Liga msimu huu

Barcelona wakomoa Valencia na kuweka hai matumaini ya kuibuka wafalme wa La Liga msimu huu

Na MASHIRIKA

BARCELONA waliweka hai matumaini ya kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu baada ya kutandika Valencia 1-0 mnamo Jumapili ugani Camp Nou.

Bao la pekee katika pambano hilo lilijazwa kimiani na Raphinha Belloli baada ya kushirikiana vilivyo na Sergio Busquets katika dakika ya 15.

Masogora hao wa kocha Xavi Hernandez walipoteza nafasi murua zaidi ya kudhibiti mchezo katika kipindi cha pili baada ya Ferran Torres kupoteza mkwaju wa penalti.

Ansu Fati alishuhudia pia kombora lake likigonga mwamba wa goli la Valencia dakika chache kabla ya beki wao Ronald Araujo kuonyeshwa kadi nyekundu.

Difenda huyo raia wa Uruguay aliadhibiwa kwa kosa la kumkabili visivyo mwanasoka Hugo Duro aliyekuwa akijaribu kuwahi mpira uliokuwa umepigwa kwa kichwa na beki Jules Kounde wa Barcelona.

Mechi hiyo ilikuwa ya 18 kati ya 24 katika La Liga kwa kipa Marc-Andre ter Stegen wa Barcelona kukamilisha bila kufungwa bao msimu huu. Alidhibiti vilivyo jaribio la pekee kutoka kwa Valencia langoni mwake kwa kupangua fataki kutoka kwa Justin Kluivert mwishoni mwa kipindi cha pili.

Barcelona ambao sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la La Liga kwa alama 62, walikuwa bila huduma za wafungaji wao mahiri Robert Lewandowski, Ousmane Dembele na Pedri Lopez wanaouguza majeraha. Xavi naye alilazimika kutazama mchuano kutoka eneo la mashabiki ikizingatiwa kuwa alikuwa akitumikia marufuku ya mechi moja.

Valencia wanaokodolea macho hatari ya kuteremshwa ngazi, wanakamata nafasi ya 19 kwa alama 23 kutokana na mechi 24 za La Liga muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

David de Gea alegea na kukubali mabao 7 yaingie Salah...

TALANTA: Ngoi asiye na mfano

T L